Baada ya umeme kufika vijijini, sasa ni kwenye vitongoji

0

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewaambia Wananchi wa mkoa wa Kigoma kuwa, baada ya Serikali kukamilisha kazi ya kufikisha nishati ya umeme vijijini vyote kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwenye vijiji vyote, sasa msukumo unaamia kwenye kusambaza umeme kwenye vitongoji visivyo na umeme katika mkoa huo.

Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo alipokuwa katika ziara yake mkoani Kigoma katika kijiji cha Makere na Nyakitonto vilivyo katika Halmashauri ya wilaya ya Kasulu vijijini, ambapo imeelezwa kuwa kazi hiyo ya kusambaza umeme kwenye vijiji vya mkoa wa Kigoma imetekelezwa kwa mafaniko makubwa ambapo kati ya vijiji 306 vya mkoa huo, vijiji 268 vimeunganishwa na huduma ya umeme, sawa na asilimia 87.

Awali, alipokuwa katika kijiji cha Makare, Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Agustino Vuma alisema kati ya vijiji 56 vya Kasulu vijijini; vijiji 47 vimeshawashwa na kuongeza kuwa bado vijiji 9 tu ambapo ameiomba Serikali kuongeza nguvu ya kusambaza umeme kwenye vitongoji vya jimbo hilo.

“Mhe. Makamu wa Rais, nguzo zimeshafika ili kukamilisha vijiji vilivyobaki, tunaomba kasi ile ile iliyofikisha umeme kwenye vijiji iendele na kwenye vitongoji vyote vya Halmashauri ya wilaya ya Kasulu”.

“Napenda pia kuwaomba Wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu vijijini, wahamasike na wajiunganishe huduma ya umeme ili wautumie kuanzisha, miradi ya kiuchumi”. alisema Vuma.

Kwa upande wake, Dkt. Florence Samizi, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe alisema Halmashauri ya wilaya ya Kibondo umeme umefika kwenye vijiji vyote 50 na kwamba angependa kuona umeme ukifika kwenye vitongoji vya Halmashauri ya wilaya hiyo.

“Mhe. Makamu wa Rais, nakumbuka ulipokuja jimbo kwa ajili ya kuniombea kura za ubunge, kwenye uchaguzi wa Mbunge mwaka 2021; changamoto kubwa Jimbo la Muhambwe ilikuwa ni umeme, kati ya vijiji 50, ni vijiji saba tu (7) ndivyo vilivyokuwa, vimefikiwa na huduma ya umeme, leo hii, vijiji vyote hamsini, vimefikiwa na huduma ya umeme na sasa wameanza kwenye vitongoji”. alisema, Dkt. Samizi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here