Walioipaisha Tanzania kitehama duniani wapokewa kishujaa

0
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Tume ya Tehama, Sadath Kalolo (wa kwanza kushoto) aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Nkundwe Mwasaga, akiwa katika mapokezi ya vijana wa Kitanzania waliong’ara na kutwaa ushindi wa dunia katika mashindano ya Tehama yanayoandaliwa na Huawei, jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam. Katikati ni Profesa Baraka Maisela wa Ndaki ya Tehama ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kulia ni Mkuu wa Mawasiliano wa Tume ya Tehama, Eric Mkuti. (Picha kwa hisani ya Tume ya Tehama).

*Waziri Nape awapa `Tano’, kukutana nao rasmi
*Tume ya TEHAMA yaahidi kukuza bunifu za TEHAMA

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeahidi kuboresha mazingira ya kukuza bunifu za teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa kujenga vituo vinane vya kukuza bunifu za TEHAMA nchini ili kuhakikishia Watanzania hawaachwi nyuma na kasi ya ukuaji wa TEHAMA.

Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Mhandisi Sadath Kalolo aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Nkundwe Mwasaga wakati ya mapokezi ya vijana wa Tanzania walioibuka washindi wa tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya Huawei (Huawei ICT Competition), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Vijana hao, Dickson Mram, Matimu Mahimbo na James Magessa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliwabwaga washiriki wengine 470 kutoka zaidi ya nchini 49 zilizovuka hatua za awali za ushindani. Katika fainali walichuana kwa ubunifu na mafunzo ya vitendo kwa siku tatu kuanzia Mei 23 huko Shenzhen, China.

Mashujaa wa Tehama kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakiwa katika picha ya pamoja na Mkufunzi wao, Mhandisi Jumanne Ally ambaye ni Mhadhiri Msaidizi katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) mara baada ya kuwasili nchini jana wakitokea Chenzhen, China walikong’ara kutwaa ushindi wa dunia katika mashindano ya Tehama yanayoandaliwa na Huawei. Kutoka kulia kwa Mkufunzi ni James Amos Magessa, Matimu Mahimbo na Dickson Mram.

Alisema, ushindi huo wa kihistoria kwa vijana wa Kitanzania umelipatia taifa heshima kubwa na kutoa taswira kwamba, ushindi huu unaweka mwelekeo mzuri wa nchi yetu hasa katika kipindi hiki cha kuimarisha mabadiliko ya kidijiti na kujenga uchumi wa kidijiti.

“Ushindi wenu si ni heshima kwenu bali ni heshima kwa taifa letu. Ninyi ni mashujaa wetu. Mmeandika historia kwenye tasnia ya TEHAMA kwa sababu mashindano haya ya TEHAMA ya Huawei ni moja ya mashindano makubwa na yenye ushindani mkubwa.

“Tunawapongeza sana vijana wetu. Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, ninapenda kuwapa salamu kutoka kwa Waziri wetu wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye kwamba amefurahishwa sana na ushindi huu na ameahidi kuonana nanyi mara atakaporejea nchini,” alisema Mhandisi Kalolo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Tume ya Tehama, Sadath Kalolo (wa kwanza kushoto) aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Nkundwe Mwasaga, akikabidhi maua kwa Mhandisi Jumanne Ally, Mhadhiri Msaidizi katika Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) ambaye pia Mkufunzi wa vijana wa Kitanzania waliong’ara na kutwaa ushindi wa dunia katika mashindano ya Tehama yanayoandaliwa na Huawei, jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam. (Picha kwa hisani ya Tume ya Tehama)

Aliongeza kuwa, vituo vitakavyotumika kukuza bunifu za TEHAMA vitajengwa kwenye Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Lindi na Mjini Magharibi, kwa upande wa Zanzibar.

Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa karibu zaidi na vyuo vikuu nchini, na wadau wengine kwenye sekta ya TEHAMA wa ndani na nje ya nchi, lengo likiwa ni kuhakikisha kasi ya ujenzi wa Uchumi wa kidigitali inapata msukumo wa karibu na pia kuifanya iwe shirikishi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here