NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deogratius Ndejembi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan tayari ameidhinisha kutolewa kwa fedha za dharura za barabara za TARURA kiasi cha Shilingi Bilioni 30.
Ndejembi alitoa kauli hiyo katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara na Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambapo ameambatana na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kutembelea miundombinu iliyoathirika na mvua zinazoendelea kunyeesha nchini.
Katika ziara hiyo, Ndejembi amewaelekeza Mameneja Mikoa wa TARURA nchi nzima kufanya tathimini ya uharibifu wa miundombinu iliyotokea kwenye maeneo yao na kwa haraka waanze hatua za matengenezo ya miundombinu hiyo ili kuondoa adha inayowakabili wananchi.
“Nitoe pole kwa wananchi wa maeneo haya ambayo mvua hizi zimeleta changamoto ya kuharibika kwa miundombinu, lakini niwatoe hofu kuwa barabara zote za TARURA tayari Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameshaidhinisha Shilingi Bilioni 30 kwa ajili ya matengenezo ya dharura nchi nzima.
Kwahiyo niwatake mameneja wa mikoa wote kufanya tathimini ya uharibifu uliotokea kwenye maeneo yao na hatua za haraka za kutatua changamoto hizo zianze mara moja ili wananchi wetu waweze kuendelea na shughuli zao kama kawaida,” alisema Ndejembi.