Na Happiness Shayo
SERIKALI imejipanga kuboresha utendaji kazi, kuleta mapinduzi katika utoaji huduma na utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya uhifadhi wa Wanyamapori, ikiwemo utatuzi wa migongano baina ya binadamu na Wanyamapori.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki katika Maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani yenye lengo la kuamsha ari na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu uhifadhi na umuhimu wa matumizi endelevu ya rasilimali za Wanyamapori na misitu yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Stendi ya zamani, Wilayani Babati Mkoani Manyara.
Alisema, Serikali imeendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali za sekta hiyo za ujangili, biashara haramu ya nyara na mazao ya misitu, uvamizi wa maeneo ya hifadhi, shoroba na mtawanyiko wa wanyamapori, kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi na mabadiliko ya tabia nchi.
“Naomba nichukue fursa hii kuufahamisha umma wa Tanzania na dunia kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi imejizatiti katika kutatua changamoto hizi kwa kuandaa mikakati ya kuzikabili” alisisitiza Kairuki.
Waziri Kairuki ameitaja mikakati hiyo kuwa ni Mkakati wa Kutekeleza Sera ya Wanyamapori wa Mwaka 2023 – 2033, Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ujangili wa Mwaka 2023 – 2033, Mpango Mkakati wa Kupambana na Wanyamapori wakali na Waharibifu wa Mwaka 2020 – 2024, Mpango Mkakati wa Kuongoa Shoroba wa Mwaka 2022-2026 na Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi wa Maeneo ya Jumuiya za Wanyamapori za Jamii wa Mwaka 2023 – 2033.
Sambamba na hilo, alisema katika kuhakikisha kuwa urithi wa Wanyamapori unalindwa ili uendelee kutoa mchango wake katika uchumi na maendeleo ya jamii, Tanzania iliridhia Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyo hatarini Kutoweka (Convention on International Trade in Endangered Species of Wild Fauna and Flora-CITES) Mwaka 1979 na kuanza kutumika rasmi Mwaka 1980 kwa lengo la kudhibiti biashara ya Kimataifa ya Wanyamapori na Mimea iliyo hatarini kutoweka ili isiathiri ustawi wao.
Aidha, Kairuki alisema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha usimamizi, ulinzi na uhifadhi maliasili ikiwa ni pamoja na kuimarisha Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Kikosi Kazi cha Taifa Dhidi Ujangili ili kudhibiti ujangili wa wanyamapori na misitu.
Pia, amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inashirikiana na Wizara nyingine za kisekta katika kuandaa na kusimamia mipango ya matumizi ya ardhi nchini ili kupunguza uvamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria pamoja na Shoroba za Wanyamapori.
Waziri Kairuki aliongeza kuwa, mbinu nyingine za kukabiliana na changamoto za sekta ya uhifadhi wa wanyamapori ni kuhamasisha wananchi kuanzisha maeneo ya ufugaji wa Wanyamapori (Ranchi, Mashamba, Bustani) ili kujiongezea kipato na kushiriki kikamilifu katika uhifadhi na kuanzisha maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori Jamii (WMA), hasa katika maeneo yenye changamoto kubwa ya Wanyamapori wakali na waharibifu.
Aliongeza kuwa, Serikali pia inaendelea kushirikiana na wadau wengine katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kushirikiana na Halmashauri za Wilaya kuandaa na kutekeleza matamasha mbalimbali ya uhifadhi na utalii kwa lengo la kuhamasisha shughuli za utalii nchini akitolea mfano wa tamasha lililofanyika Wilayani Same hivi karibuni – SAME UTALII FESTIVAL.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na -Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dastan Kitandula, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, CP Benedict Wakulyamba, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Wanyamapori, Dkt. Fortunata Msoffe, Makamishna wa Uhifadhi wa TAWA, TANAPA, NCAA na TFS, Mkurugenzi wa Halmashauri, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa kidini, Wakuu wa Idara na Taasisi, Maafisa na Askari wa Uhifadhi na Wadau wa Wizara ya Maliasili na Utalii;