Na Albano Midelo, Songea
MRADI wa Global Partnership for Education (GPE) utaongeza fursa ya upatikanaji wa Elimu bora kwa watoto kuanzia ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Elimu maalum na Elimu kwa walio katika mfumo usio rasmi hususan wanaotoka katika mazingira hatarishi.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Jumanne Mwankhoo wakati akifungua kikao cha (GPE) kilichofanyika katika Ukumbi wa Hospital ya Rufaa ya Mkoa, Songea.
Serikali kupitia mradi huo inatarajia kuajiri walimu wa kujitolea 600 ambao watalipwa kila mwezi Shilingi laki tatu na kwamba mradi huo wa miaka miwili unatekelezwa kwa ufadhili wa Shilingi Bilioni 212.
Mwankhoo alisema, kupitia mradi huo Serikali itaboresha mazingira ya walimu kwa kujenga nyumba za walimu katika maeneo ya pembezoni na kuwahamasisha walimu kwa kuwapa motisha.
“Mradi wa GPE unatoa ufadhili wa masomo kwa walimu wanaofundisha elimu maalumu ili kuwajengea uwezo mkubwa zaidi katika kazi”, alisema Mwankhoo.
Amelitaja lengo la mradi huu kuwa ni kuimarisha mfumo wa motisha kwa walimu wanaofundisha shule za pembezoni na kutekeleza mpango wa ajira kwa walimu wa kujitolea ambapo zaidi ya walimu 600 wataingizwa katika mradi huo na kupewa posho ya shilingi laki tatu kwa mwezi.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dionice Lukweme amesema mradi huo umekuja na mfumo ambao utawezesha kuwasimamia walimu watakaokuwa wanajitolea katika shule.
Alisisitiza kuwa, kupitia mfumo huo watakuwa na takwimu ya walimu wote wanao jitolea katika shule zote nchini.
Kwa upande wake Mwezeshaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Eva Mosha alisema, mradi unatengeneza mazingira rafiki ya kufundisha na kujifunza Kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na walimu,
Alibainisha zaidi kuwa, mradi huo unafadhiliwa kwa Dola za Marekani Milioni 84 ambazo ni zaidi ya Shilingi Bilioni 212 ambapo amekitaja kipaumbele cha kwanza ni kujenga nyumba za walimu katika Halmashauri ambazo zipo pembezoni.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mfaranyaki Zuhura Nikata alisema, mradi huu utatatua changamoto za walimu kwa asilimia 90 kwa kuwa utawajengea walimu makazi jirani na vituo vyao vya kazi na kutoa posho kwa walimu wanaojitolea Kwa muda wa miaka miwili.
Kwa upande wake Mwalimu wa Shule ya Msingi Amani, Ayubu Ng’ombo Yahaya alisema mradi huu utawasaidia walimu kupata mbinu mpya za kufundishia na kuhamia katika mfumo wa kisasa wa kijiditali.