MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango amewasha umeme katika Kituo cha Afya Ketumbeine, kilichopo katika kijiji cha Armanie wilayani Longido, Mkoa wa Arusha na kupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusambaza nishati hiyo kwa ufanisi.
Akizungumza na umati wa wananchi katika uwanja wa Kituo cha Afya Ketumbeine baada ya kuwasha umeme na kukizindua rasmi, Dkt. Mpango alisema azma ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwapelekea wananchi maendeleo inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi na Serikali anayoiongoza.
“Nimefika hapa, kwanza tumewasha umeme kwa ajili ya kituo hiki cha Afya. Napenda niwapongeze sana watu wa REA kwa kazi nzuri. Sasa Kituo chetu cha Afya, nina hakika wananchi watakaokuja kupata huduma hapa watapata huduma ya uhakika,” alisema.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Arusha, mbele ya Makamu wa Rais, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alisema Serikali kupitia REA imewekeza jumla ya Shilingi Bilioni 73.9 kwa Mkoa huo.
Alisema, fedha hizo ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi mitano ya umeme vijijini ambapo jumla ya vijiji 263 kati ya 268 vya Mkoa wa Arusha vimekwishafikishiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, ikiwa ni asilimia 71.46.
Mhandisi Saidy aliongeza kuwa, vijiji vilivyosalia vitaendelea kupelekewa umeme kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA na kwamba ifikapo Juni mwaka huu, vijiji vyote vitakuwa vimekwishafikiwa.
Ameitaja miradi mingine inayoendelea kutekelezwa na REA mkoani Arusha kuwa ni REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B, Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Migodi midogo na maeneo ya kilimo pamoja na Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.
Akifafanua zaidi, amesema kuhusu Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu, fungu la Kwanza limekamilishwa kwa asilimia 61 likihusisha uwashwaji wa vijiji 27 kati ya 44; na la Pili limekamilika kwa asilimia 95 likihusisha uwashwaji wa vijiji 58 kati ya 61.
Akizungumzia malengo ya kutekeleza Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B, Mkurugenzi Mkuu ameeleza kuwa unalenga kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha ambapo wigo wa kazi unahusisha kuyafikishia umeme maeneo 81 kwa gharama ya shilingi Bilioni 11.
Kwa upande wa Mradi wa kupeleka umeme katika Migodi midogo na maeneo ya kilimo, wigo wa kazi unalenga kuifikia migodi na maeneo ya kilimo 27 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.5.
Aidha, Mhandisi Saidy alisema, Mradi wa kupeleka umeme katika Taasisi za Afya na Pampu za Maji unalenga kupeleka umeme katika maeneo hayo ambayo hayajafikiwa ili kupambana na magonjwa ya mlipuko ukiwemo UVIKO-19.
“Wigo wa kazi unahusisha kupeleka umeme katika pampu za maji 17 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.5 na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 9 ambapo kazi ya ujenzi imefikia asilimia 97.”
Tukio la kuwasha umeme na kuzindua Kituo cha Afya limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, Maafisa wa Serikali pamoja na wananchi.