Na Abel E. Kiharo
SIKU moja kuna mtoto alivunja sahani wakati wa kuosha vyombo vya chakula. Mzazi wake alipomuuliza sababu ya kuvunjika kwa sahani hiyo, mtoto alijibu ‘ni bahati mbaya.’
Kilichofuata baada ya hapo, ilibidi mzazi amchukue yule mtoto ili wakamtafute huyo bahati mbaya, ambaye ndiye chanzo cha sahani ile kuvunjika.
Hii inaonesha wazi neno ‘bahati mbaya’ lilikuja kama kisingizio cha kumfanya mtu aonekane hana hatia. Huenda sababu ilikua ni uzembe ulioambatana na kukosa umakini kwa mtoto huyo, lakini aliamua kutoa sababu hiyo ambayo huenda ikamfanya asijirekebishe.
Unahitaji kuuvuka mstari wa mazoea ili uweze kuufikia ushindi mkubwa maishani mwako. Ili upate matokeo ambayo siyo ya kawaida ni lazima ukubali kuanza kufanya mambo kwa namna ambayo si ya kawaida.
Mtu mmoja mwenye hekima aliwahi kunukuliwa akisema: “Hauwezi kuyapata matokeo tofauti kwa kuendelea kufanya mambo kwa namna ile ile ambayo imekupatia matokeo haya uliyo nayo sasa”.
Kupata kilicho bora anza kufanya kwa namna iliyo bora, kupata kilicho cha kipekee anza kufanya kwa namna ya kipekee na kufika mbali anza kwa kuona mbali. Inawezekana kabisa unatamani upate ushindi mkubwa maishani mwako, lakini ni kweli unafanya mambo kwa namna ya kuundaa ushindi huo?
Kama unataka upate matokeo yaliyo bora maishani mwako hakikisha unakuwa tayari kulipa zile gharama zitakazokupatia matokeo hayo.
Kama unataka kuyafanya maisha yako yaonekane kwa namna ya kitofauti anza kwa kuyakataa mazoea kwa njia ya kufanya mambo kwa namna ya tofauti. Kutoka kuamini kuna bahati mbaya mpaka kuamini kila jambo ni matokeo ya gharama fulani iliyolipwa.
Kila jambo lipo kwa namna ambayo ili kulipata, yakupasa kufuata utaratibu fulani. Mfano, kama unataka kunywa maji ambayo yapo bombani, ili uyapate ni lazima ukubali kuinuka na kulifuata bomba lilipo.
Hii huitwa ulipaji wa gharama, ambapo tunaambiwa kuwa, kwa jambo lolote unalolihitaji katika maisha yako, inakuhitaji kulipa aina fulani ya gharama kwanza ili ulipate jambo hilo. Hii ni kusema kwamba, hakuna jambo la bure hapa duniani!
Matokeo ya aina yoyote unayoyaona sehemu ni matunda ya gharama fulani iliyolipwa. Kwa sehemu kama matokeo hayo ni mazuri, kuna gharama ya juhudi na umakini ililipwa mahali hapo na kama ni mabaya, basi inawezekana kuna gharama ya uvivu na kukosa umakini imelipwa hapo.
Kama unataka kufaulu sana masomoni, gharama yake ni kusoma kwa bidii na umakini mkubwa, kama unataka uwe na afya njema gharama yake ni kuutunza vyema mwili wako, kama unataka uzifikie ndoto zako gharama yake ni kufuata njia sahihi itakayokufikisha kwenye ndoto hiyo huku ukiwa umejitoa kikamilifu kwa akili na nguvu zako zote.
Duniani hakuna kitu cha bure na hakuna kinachotokea hapa duniani kwa bahati mbaya! Hii ni siri ambayo unapaswa kuielewa na kuanza kuiishi sasa.
Kuamini kuna vitu utavipata bure pasipo kulipa gharama ya aina yoyote ni kujidanganya na kufikiri kuna mambo hututokea maishani mwetu kwa bahati mbaya, hapo ni kutafuta visingizio. Kila matokeo ni matunda ya visababishi na kila faida ni matokeo ya gharama iliyolipwa.
Kuna taratibu mbalimbali maishani mwako ambazo ni lazima uzivunje sasa, ili kwamba uweze kupata kilicho bora zaidi katika maisha yako. Kuna mila na desturi ambazo ni lazima ukubali kuziondoa katika fikra zako ili uanze kuyaona maisha yako na dunia tuliyonayo kwa jicho la utele.
Esta ili kuikomboa nchi ya Israel ilimlazimu kwenda kinyume na utaratibu, na kama asingefanya hivyo kuna uwezekano mkubwa Waisraeli wote wangeangamizwa.
Kwenda kinyume na utaratibu, inawakilisha kwenda kinyume na mazoea au u-kawaida. Tusipo kubali kwenda kinyume na mazoea kuna ndoto zetu kubwa zitaangamia na kusababisha hata ndoto za wengine wengi ziangamie pia.
Tusipo kubali kuanza kufanya mambo kwa namna ambayo si ya kawaida, namna ambayo ni tofauti na hii ambayo imetuletea haya matokeo ya kawaida katika maisha yetu, kwa hakika tutaendelea kuishi maisha ambayo ni ya kawaida mno.
Mkulima hawezi kupata mavuno tofauti na yale aliyoyapata msimu uliopita ikiwa atalima sasa kwa namna ile ile ya msimu uliopita. Ni lazima ukubali kuuvuka mstari wa mazoea, ni muhimu ukubali kuuchukia ukawaida.
Malengo yangu makuu ya kukuandikia makala hii ni haya yafuatayo:- Mosi, Ubadilishe mtazamo wako kutoka kuamini kuna vya kupatikana bure hapa duniani mpaka kuamini kila kitu hutokea baada ya maandalizi fulani kufanyika.
Pili, kwa kuwa kila matokeo huja baada ya kusababishwa basi hakuna ‘bahati mbaya’ katika maisha yetu. Kuiendekeza bahati mbaya ni kuendekeza visingizio, yani kutafuta sababu za kujitetea ili tuonekane hatuna hatia yoyote juu ya aina ya maisha tuliyonayo sasa.
Pale utakapoweza kuyaelewa vyema mambo hayo mawili, maisha yako yataanza kubadilika kwa kasi ya ajabu. Hivi unafahamu kama ukiwa ni mtu wa kupenda sana vya bure, itakufanya hata wewe uonekane ni wa bure kutokana na maisha yako kukosa thamani?
Ukweli ni kwamba, thamani ya maisha yako huongezeka pale unapokuwa unayafanya yale mambo yanayokufanya uonekane wa tofauti na wengine. Mfano, thamani yako itaonekana vipi kwa kuwapatia maji wale watu wanaoishi mtoni?
Pale maisha yako yanapokuwa chini kuna mambo yamefanyika, ambayo yamekusukumia chini na pale maisha yako yanapoonekana kuwa juu, elewa kuna mambo umeyafanya ambayo yamefanya maisha yako yainuke.
Hivyo, unapaswa kuwa makini na yale mambo unayoyafanya sasa, ikiwa utajikita na kufanya yaliyo bora sasa, waandaa matokeo bora hapo baadae na ikiwa unafanya yaliyo mabaya sasa; basi elewa moja kwa moja hapo unaandaa matokeo yaliyo mabaya hapo baadae!
*Mwandishi wa Makala hii ni Mwandishi, Mkufunzi wa Vijana na Mjasiriamali. Kwa maoni, ushauri au maswali usisite kuwasiliana naye kwa anuani zifuatazo:- Barua pepe: kiharoabel@yahoo.com. WhatsApp na Simu ya kawaida: +255767180002/+255628733839. Mitandao ya kijamii: https://linktr.ee/abelkiharo.