Rais Mstaafu JK atembelea shule za Msingi Dar

0

Na Jumbe Abdallah

MWENYEKITI wa Bodi ya Mfuko wa Kusaidia Maendeleo ya Elimu Duniani (GPE), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Laura Frigenti wametembelea na kukagua shule za Msingi ya Maji Matitu iliyoko Mbagala na Mikongeni iliyoko Gongo la Mboto jijini Dar es salaam.

Ziara hiyo, ambayo Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omary Juma Kipanga na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Deo Ndejembi pia walikuwepo imefanyika siku tatu kabla ya mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi wa GPE utakaofanyika Zanzibar kuanzia mapema wiki ijayo.

Dkt. Kikwete, akiwa Mwenyekiti wa GPE ataongoza vikao hivyo kuanzia Disemba 4 hadi 6, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa Shirika hilo la Kimataifa kufanya vikao vyake vya bodi barani Afrika.

Madhumuni ya ziara hiyo ilikuwa ni kukagua na kujionea shule ambazo Shirika hilo limetoa ufadhili.

Katika shule ya Maji Matitu shirika hilo limefadhili ujenzi wa madarasa nane na matundu 20 ya vyoo, wakati katika shule ya Mikongeni imechangia ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo.

Akiongea baada ya ziara hiyo, Dkt. Kikwete ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na GPE katika kuboresha sekta ya elimu hasa hasa kwa wasichana na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi na mikakati ya kuiendeleza sekta hiyo.

Dkt. Kikwete, ambaye ni Mwafrika wa kwanza kuongoza GPE, alisema shirika hilo hadi sasa limeishaipatia Tanzania jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 332 (takriban shilingi 834,980,332,000.00) ili kusaidia sekta ya elimu bara na visiwani.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE Bi. Frigenti ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kuendelea kusaidia juhudi za kuendeleza sekta ya Elimu hususani katika nchi zenye uhitaji, akisisitiza kwamba changamoto nyingi za kimaisha zinaweza kuepukika endapo wananchi watapatiwa elimu bora.

Frigenti ameeleza kuridhishwa kwake na matumizi ya Fedha ambayo GPE imekuwa ikitoa kwa Tanzania na kusema kuahidi kuendeleza uhusiano mzuri uliopo na uliodumu kwa miaka 10 sasa.

Aidha, ameisifia Serikali kwa kuendelea na juhudi zake za kuendeleza elimu kwa kujenga miundo mbinu bora na kuhakikisha kila mtoto anapatiwa elimu.

Novemba mwaka huu, GPE imetiliana saini na Serikali ya makubaliano ya kutoa dola za Kimarekani milioni 85 (takriban shilingi 213, 775, 085, 000.0) kwa ajili ya kusaidia mafunzo ya walimu nchini.

GPE iliyoanzishwa mwaka wa 2002, ni Shirika linalosimamiwa na Benki ya Dunia, linalofadhili maendeleo ya elimu ya msingi na utendaji wa sera za nchi zinazoendelea.

Majukumu ya GPE ni pamoja na kusaidia Serikali za nchi zinazoendelea kufanya mabadiliko ya kimfumo na kuoanisha rasilimali na ufadhili ili kutoa elimu bora kwa watoto Wote, kuinua viwango vya kujifunza na kukabiliana na changamoto mpya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here