Wakili Kaluwa azidi kujiimarisha mbio za Uenyekiti Simba

0
Wakili Moses Kaluwa akisisitiza jambo wakati akinadi sera zake kwenye moja ya matawi ya wanachama wa Simba, jijini Dar es Salaam.

Na Andrew Chale, Dar es Salaam

WAKILI msomi na Mwanasheria, Moses Kaluwa ameendelea kujiimalisha kwa kunadi sera zake katika matawi mbalimbali zaidi ya 30, ikiwemo Jijini Dar es Salaam na Mikoani ikiwa ni hatua ya mwisho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Simba Januari 29, ukumbi wa JNICC.

Akiwa katika mwendelezo wa kampeni hizo mapema leo Januari 27, katika matawi ya Dar es Salaam, amekutana na matawi zaidi ya Sita (6) ya Wanachama wa Simba yakiwemo ya Simba Dume la Mwembe chai, Wekundu wa Terminal (Mbezi mwisho), Vuvuzela la Mwananyamala, Mdomo wa Simba na mengineyo.

Kaluwa katika kampeni hizo, amenadi vipaumbele vyake mbali mbali huku akiahidi kushirikiana na viongozi wengine pamoja na Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji Mo, na Wanachama wote wa Simba nchi nzima na nje ya nchi.

Wakili Moses Kaluwa ambaye ni mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Simba akiwasili kwenye moja ya matawi ya Simba kunadi sera zake.

“Vipaumbele vyangu ni pamoja na kushirikiana na matawi yote nchi nzima. Pia, kubuni miradi kwa kushirikiana na Mwekezaji na wadhamini wa ndani na nje. Kuhakikisha bodi inakuwa na uendelezaji wa miundombinu ya viwanja vya mazoezi na mechi,” alisema Kaluwa.

Akiendelea kunadi vipaumbele vyake Kaluwa alisema: “nitahakikisha tunaendeleza miradi ya vipaji vya Watoto na vijana, kujenga mbinu za kuongeza hamasa, kuajiri watalaam wa kila eneo ilikuwezesha timu kupata matokeo.”

Mbali na hayo, Kaluwa alisema atahakikisha kwa kushirikiana na viongozi wenzake, Simba inaongeza mapato zaidi na kudumisha utamaduni ulijengwa na waanzilishi wa klabu hiyo kongwe.

“Nitahakikisha tunaenzi na kudumisha mila, desturi na tamaduni zilizoasisiwa na Wazee wetu ambao ni waanzilishi wa klabu yetu ili ziendelezwe na vizazi vijavyo,” alisema Kaluwa.

Wakili Kaluwa akizungumza na wanachama wa Simba kwenye tawi la Wekundu wa Terminal.

Vile vile Kaluwa ambaye ananadiwa na Mwenyekiti wa zamani, Hassan Dalali na wanachama wa Simba wa matawi mbalimbali alisema, atahakikisha anajenga, kuyalinda, na kuyaenzi Mahusiano mazuri yaliyopo kati ya mashabiki, Wanachama, Mwekezaji na wadhamini kwa kila eneo kwa Maendeleo ya Simba.

Katika hatua nyingine, wagombea wanaowania nafasi mbalimbali ndani ya klabu ya Simba akiwemo Eng Rashid Mashaka ambaye ni mgombea wa Ujumbe Bodi ya Ukurugenzi, wamenadi sera zao ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here