Saudi Arabia yaishangaza Dunia kwa kuichapa Argentina

0
Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Saudi Arabia, wakishangilia ushindi wao wa kihistoria wa bao 2-1 dhidi ya Argentina ya kina Lionel Messi, kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Qartar

Na Rama Msangi

MFALME Salman wa Saudi Arabia, ametangaza jumatano ya Novemba 23 kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa, ili kutoa nafasi kwa wananchi wake kusherehekea ushindi wa 2-1 ambao timu yao ya taifa imeupata leo hii dhidi ya Argentina, katika michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Qartar.

Lionel Messi, anayetajwa kuwa hizi zitakuwa fainali zake za mwisho huku pia taifa lake likiwa miongoni mwa yanayotajwa kuwa na kikosi bora kabisa katika mashindano haya, aliipatia timu yake bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti kunako dakika ya 10 tu ya mchezo na hapo dunia ikaanza kudhani kuwa jambo pekee wanaloweza kufanya Saudi Arabia, ni kujipanga kudhibiti ukubwa wa madhara tu katika mechi hiyo.

Hata hivyo, wa-Saudia wenyewe walikuwa na kitu tofauti vichwani mwao.

Mabao mawili ya haraka haraka yaliyopatikana mwanzoni mwa kipindi cha pili, yakiwekwa kimiani na Al Shehri (dakika ya 48 na lile la Al Dawsari (53) yakapelekea kile ambacho kimeshaingia katika kumbukumbu za vitabu vya soka duniani, kama moja ya matokeo ya kushtusha sana kuwahi kutokea katika mchezo huo.

Saudi Arabia, ni moja ya mataifa yaliyo karibu sana na Qatar, zinakofanyika fainali hizo, na wapo watu wengi tu ambao walisafiri kwenda kushuhudia mechi hiyo. Wa mbali kabisa walisafiri kwa saa tatu kufika uwanjani. Lakini timu yako inapokupa matokeo kama haya, ni wazi kabisa kuwa umbali unabaki kuwa namba tu, mbele ya furaha kubwa anayokuwa nayo shabiki.

Kwa mashabiki wengi wa soka, ushindi wa Saudi Arabia unaweza kuchukuliwa kama moja ya zile “fluke” za kwenye soka, lakini kwa wafuatiliaji wa karibu sana wa kikosi hicho, bila shaka watakuwa wanajua kuhusu mtu anaitwa HervĂ© Renard, na wanaomfuatilia sana raia huyu wa Ufaransa, watakwambia kuwa huyu ndio “Mchawi katika Timu ya Soka ya Saudi Arabia”

Kocha huyu aliyezaliwa mwaka 1968, anakumbukwa kwa kuiwezesha timu ya taifa ya Zambia kubeba Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) katika fainali za mwaka 2012, kabla ya kurejea tena mafanikio hayo miaka mitatu baadae akiwa na kikosi cha Ivory Coast.

Naam, ni huyu ambaye amekiongoza kikosi cha Arabie Saoudite, kuwaadhiri akina Lionel Messi, Angel de Maria na mafundi wengine kibao waliosheheni kwenye kikosi cha Argentina. Na kwa ushindi huo, Saudia, wanaongoza kundi lao kwa kuwa na alama 3, huku Argentina wakiwa mkiano na alama 0. Poland na na Mexico ambazo zinakamilisha kundi hilo, zina alama moja moja, baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika pambano lililowakutanisha.

Swali la je, “mchawi” Herve, ataiongoza Saudia kufanya maajabu hadi wapi, pengine litajibiwa na muda zaidi, na kwamba ni muda gani, hilo hakuna anayejali kwa sasa. Kile wananchi wa Saudia, na wenzao kote duniani ambao hawaipendi Argentina, wanafanya kwa sasa, ni “kuvuta kwa furaha” kila pumzi iliyoletwa na ushindi wao huu mkubwa katika historia ya nchi yao

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here