Serikali yaahidi kutopandisha nauli ya Treni Mikoa ya Kaskazini

0

Na Jumbe Abdallah

SERIKALI imewahakikishia wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Arusha kuwa hakutakuwa na ongezeko la nauli ya treni inayopita katika mikoa hiyo ili kuwawezesha kufanya safari zao kwa urahisi hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.

Akizungumza jijini Arusha, mara baada ya kutembelea Stesheni ya reli ya kati Naibu Waziri Mwakibete alisema, uwepo wa treni hiyo umerahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo baina ya Dar es Salaam na mikoa hiyo na hivyo Serikali inatarajia kuongeza idadi ya mabehewa ili kuwawezesha abiria wengi zaidi kutumia usafiri huo.

“Toka kuanzishwa kwa safari za treni kwa mikoa hii mwaka 2020 kumekuwa na ongezeko kubwa la abiria na mizigo na kazi ya Serikali ni kutoa huduma, hivyo niwahakikishie wananchi kuwa Serikali itaendelea na nauli zile zile pamoja na ongezeko la abiria ili kuwawezesha kuweza kwenda kusalimia ndugu zao mwisho wa mwaka,” alisema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete alisema, safari za treni zinatarajiwa kuongezeka kutoka safari  tatu (3) kwa wiki mpaka safari nne (4) kwa wiki mara mabehewa mapya yatakapowasili mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.

Aidha, aliongeza kuwa Serikali kupitia Shirika la Reli Nchini (TRC) inaendelea na ukarabati wa mabehewa takribani 600 lengo likiwa ni kuhakikisha kuna mabehewa ya kutosha ya kusafirisha abiria na mizigo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa TRC, Focus Sahani alisema, kwa sasa kupitia treni hiyo wameweza kusafirisha zaidi ya tani 11,600 za mizigo na ambao husafirishwa kwa safari moja ni zaidi ya 300.

Sahani aliongeza kuwa, kuanza kwa treni hiyo kumeleta mafanikio kwani wananchi wamepata ahueni ya kupungua kwa bei ikiwemo saruji kushuka kutoka Shilingi 20,000/- kwa mfuko mmoja mpaka Shilingi 15,000/-

Naibu Waziri Mwakibete yuko mkoani Arusha kwa ziara ya siku mbili kukagua miradi ya maendeleo na kuangalia utendaji wa taasisi zilizo chini ya Sekta ya Uchukuzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here