‘Vishikwambi vitumike kuhamasisha matumizi ya TEHAMA’

0

Na Fred Kibano – OR TAMISEMI

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amezindua zoezi la ugawaji wa vishikwambi kwa walimu wa ngazi zote ili kuboresha utoaji wa elimu kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Waziri Mkuu Majaliwa alizindua zoezi hilo hivi karibuni katika Ukumbi wa jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba nje kidogo ya Jiji la Dodoma wakati akitoa hotuba yake na kugawa vishikwambi kwa walimu wa ngazi zote wakiwemo wakufunzi wa vyuo na kuagiza kwamba ni lazima vitumike kama azma ya Serikali ilivyokusudia ya kuhamasisha na kuboresha TEHAMA katika Ufundishaji na Ujifunzaji nchini.

“Kumekuwa na uhitaji wa vifaa vya TEHAMA katika shule zetu hasa walimu wetu katika maandalizi hayo ya ufundishaji na Ujifunzaji pamoja na usimamizi, upimaji na tathmini katika Sekta ya elimu nchini” alisema Majaliwa.

Alisema, lengo la kuzindua ugawaji wa vishikwambi kwa walimu wote nchini ni kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kupitia TEHAMA, lakini hatapenda kuona vishikwambi hivyo vinakwenda kwa watu wasio walengwa.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa aliziagiza Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Sayansi na Teknolojia ya habari kutoa mafunzo ya matumizi ya vishikwambi kwa walimu na kwamba vitakuwa ni mali ya mwalimu mwenyewe, lakini pia hatapenda kuona vinazagaa mitaani.

Akitoa neno kabla ya hotuba ya Mgeni rasmi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda alisema, jumla ya vishikwambi 300,000 vilinunuliwa na Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ambapo baadhi vilitumiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), vishikwambi 6,600 vilitumika upande wa Zanzibar na vishikwambi 293,400 Tanzania Bara ambapo vilivyotumika Tanzania Bara vinagawiwa kwa walimu wa ngazi mbalimbali.

Prof. Mkenda ameyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na walimu wa shule za msingi za Serikali (185,404), walimu wa sekondari za umma (89,805), Wathibiti Ubora wa Wilaya na Kanda (1,666), Wakufunzi wa vyuo vya Ualimu (1,353), Wakufunzi wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii (297), Wakufunzi wa vyuo vya Ufundi Stadi (996), Maafisa Elimu Mkoa, Wilaya na Kata (5,772) na Baraza la Mitihani (8,357).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here