Uingereza imeiamsha dunia kwa kumchagua Rishi Sunaki – AAFP

0

. Yaelezwa ni tamati ya ubaguzi duniani

Na Mwandishi Wetu, Pemba

CHAMA cha Muungano wa Wakulima (AAFP) kimesema kumpitisha Waziri Mkuu mpya Rishi Sunaki mwenye asili ya Asia huku Mfalme Charles akiridhia, hiyo ni ishara ya ukomo wa zama za ubaguzi wa rangi duniani.

Mwenyekiti wa AAFP Said Soud Said ameeleza hayo kufuatia taifa hilo kubwa kupata Waziri Mkuu mpya ambaye katika zama za uhafidhina mkongwe na ubaguzi asingepata wadhifa huo.

Soud alisema, ni wazi dunia yote itazinduka na kuwafanya binadamu wenye fikra na mitazamo hasi kuanza kubadilika na kuacha kubaguana na kuelewa binadamu wote bila kutazama jinsia wana haki sawa.

Alisema, kutokea kwa tukio hilo huko Uingereza kumetoa somo kubwa na kuibadilisha kidunia ili iachane na siasa chafu, ambapo binadamu kwa karne nyingi walibaguana.

“Nimefurahishwa na tukio lililotokea Uingereza la kumteua Waziri Mkuu Mwingereza mwenye asili ya Asia. Taifa hilo limefikisha ujumbe mbele ya uso wa dunia na kuielekeza iachane na ubaguzi ili kujua binadamu wote ni sawa,” alisema Soud.

Aidha, Mwenyekiti huyo alisema, licha ya dunia ya siasa kuwa kitongoji kimoja kidogo, Uingereza haipaswi kubezwa kwenye Mataifa yote ulimwenguni, badala yake watilie maanani somo hilo.

“Tunajua ya kwamba kuna baadhi ya Mataifa duniani bado yako katika kiza cha dharau, maonevu, ubaguzi na kujipa utukufu. Uingereza imeshaondoka mahali huko na kuwaamsha wenye mitazamo hasi,” alisisitiza.

Soud akitoa mfano alisema, laiti ufalme wa Zanzibar usingewabagua Waafrika na kuwashirikisha katika medani za utawala, vyombo vya uwakilishi na vya maamuzi ni wazi Mapinduzi ya mwaka 1964 yasingetokea Visiwani humo.

“Waafrika wanyonge walikosa huduma za jamii kama matibabu, maji safi, barabara na umeme. Hawakuhodhi ardhi yenye rutuba kwa kuliko walime na kutopata elimu bora. Wangepata mahitaji muhimu haki na kuthamaniwa, ufalme usigeangushwa,” alisisitiza.

Aliendelea kusema: “Majengo yaliyoko mji mkongwe Zanzibar yangejengwa maeneo ya mashamba kusingekuwa na longolongo. Haiwezekani wahamiaji wale bata ugenini na wenyeji wakisaga rumba. Hapo ndipo ASP kilipoungwa mkono na watu wingi,”

Hata hivyo, Soud alisifu juhudi za vyama vya ukombozi barani Afrika, viongozi wa kisiasa, wapigania uhuru na wanaharakati kwa kusimama imara na kuhakikisha ubaguzi, ukandamizaji haki na manyanyaso yakikomeshwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here