Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Reli Tanzania- TRC limeshiriki kongamano na maonesho ya 11 ya Mashirika ya Reli katika Ukanda wa SADC (SARA RAIL conference and Exhibition 2022) yanayoendelea jijini Johannesburg nchini Afrika ya Kusini kuanzia Oktoba 26 hadi 28, 2022.
Kongamano na maonesho ya mwaka huu yamebeba ujumbe unaolenga Ubunifu katika mabadiliko ya Teknolojia za uendeshaji wa Reli, ambapo pamoja na Tanzania inayowakilishwa na TRC, Mataifa mengine ni wenyeji Afrika ya Kusini, Botswana, Eswatini, Msumbiji, Angola, DRC, Malawi na Zambia.
Akizungumza baada ya ufunguzi wa Kongamano hilo, Amina Lumuli ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TRC alisema, Tanzania imethibitisha kuwa mbele katika mipango ya mageuzi ya usafirishaji kwa njia ya Reli Kusini mwa Afrika kama ujumbe wa kongamano la mwaka huu unavyosisitiza.
“Kupitia SGR ukilinganisha na Mataifa mengine ya ukanda huu, tunaonekana tuko mbele zaidi kwa ujenzi wa miundombinu hii ya kisasa ambayo itasaidia sana katika kupunguza muda wa safari na ufanisi katika uendeshaji” alisema Amina.
Awali, akifungua Kongamano hilo, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Reli kusini mwa Afrika Siza Mzimela, ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya Usafirishaji kwa njia ya Reli katika ukanda wa SADC kuchukua jukumu la kuboresha hali ya miundombinu kwa ufanisi zaidi.
“Umuhimu wa reli katika kusukuma gurudumu la maendeleo haupingiki, na endapo njia hii ya usafiri haitaboreshwa Afrika haitaweza kuona umuhimu wa Reli katika ufanisi wa matumizi ya rasilimali zake na utajiri tuliojaaliwa” alisema Mzimela.
Aidha, ameongeza kuwa, wadau wote wanatambua hali ya uchakavu wa miundombinu na vifaa vya uendeshaji wa reli katika ukanda wa SADC na Afrika kwa ujumla, na kwasababu hiyo kunahitajika ubunifu wa mifumo ya biashara na uendeshaji ili kujikwamua na kuleta ufanisi.
Kupitia maonesho yanayoenda sambamba na kongamano hilo, Shirika la Reli Tanzania limeshiriki kuonesha juhudi na mikakati ya Serikali katika kuleta mageuzi ya usafirishaji kwa njia ya Reli.
“Kupitia ushiriki wa TRC kwenye maonesho haya tumekutana na wenzetu kutoka nchi mbalimbali, kuanzia mashirika yanayotoa huduma kama za TRC mpaka makampuni yanayotengeneza vifaa vinavyotumika katika uendeshaji wa Reli, kwahiyo kwetu imekuwa ni fursa ya kukutana na wadau wapya lakini pia kuona wenzetu wanafanya nini, au wao kujifunza kutoka kwetu,” alisema Mkuu wa Kitengo cha Habari TRC Jamila Mbarouk.
Pamoja na mashirika ya Reli, makampuni mbalimbali ya utengenezaji vifaa vya uendeshaji, teknolojia ya Reli, mitambo na vifaa vya usalama kazini, yameshiriki kongamano la mwaka huu.