Madaktari bingwa kutoka Ireland wapiga kambi MOI

0

Na Mwandishi Wetu, DSM

TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili –MOI imepokea jopo la madaktari bingwa wa mifupa wa watoto kutoka Taasisi ya ‘Children Health Ireland Africa’ ambapo wataendesha kambi maalum ya upasuaji kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa MOI kwa siku nne.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface alisema, ujio wa madaktari bingwa kutoka Ireland ni sehemu ya mkakati wa MOI wa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Kimataifa ili kuboresha huduma kwa wananchi.

“Leo tumepokea wageni kutoka nchini Ireland ambapo watakua nasi hapa kwa siku nne ambapo watatoa huduma kwa wagonjwa ikiwemo upasuaji kwa watoto 10 wenye viungo vilivyopinda,” alisema Dkt. Boniface.

Dkt. Boniface alisema, ushirikiano kati ya Taasisi ya MOI na CHIA utajikita katika maeneo ya Mafunzo, kubadilishana watumishi, utafiti, tiba mtandao pamoja na vifaa tiba.

Afisa uendeshaji Mkuu wa Shirika la ‘Children Health Ireland Africa’ Joe Gannon alisema, ni heshma kubwa kupata fursa ya kushirikiana na hospitali ya MOI ili kuangalia namna bora ya kuboresha huduma kwa watoto.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi ya CHIA Dkt. Paula Llelly alisema ushirikiano kati ya Taasisi yake na MOI utakua na manufaa makubwa kwa pande zote mbili ambapo wanufaika wakubwa watakuwa wagonjwa.

Katika kutekeleza kwa vitendo agizo la Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mh Rais Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi,

Taasisi ya MOI imekua ikianzisha ushirikiano na Taasisi mbalimbali za kimataifa ili kuboresha huduma zake kwa watanzania na kumaliza rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here