Chongolo awaonya wanaojihusisha na ‘miundombinu’ haramu

0

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameonya baadhi ya wanachama wanaotengeneza kitu alichokiita ni ‘miundombinu’ haramu.

Mtindo huo unahusisha vitendo vya rushwa, fitna na majungu ili kuwadhibiti watu bora wenye sifa nzuri za kuchaguliwa kuwa viongozi wasipate nafasi ya kushika dhamana za uongozi ndani ya chama.

Katibu Mkuu Chongolo alisema hayo Kigamboni, jijini Dar es Salaam, baada ya kuweka jiwe la msingi katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Kigamboni pamoja na kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya makazi ya Katibu wa Chama Mkoa wa Dar es Salaam, unaoendelea katika eneo la Somangila, Kigamboni.

Chongolo alisema, CCM iko makini na inafuatilia kwa karibu mchakato wote wa uchaguzi katika ngazi zote za muundo wa chama, ambao sasa umefikia ngazi za mikoa, ili kudhibiti vitendo vyote vya ukiukwaji wa taratibu, vikiwemo vitendo vya rushwa.

Alisema, chama hakitasita kuchukua hatua kali, kama kilivyofanya kwenye ngazi ya wilaya, ambapo baadhi ya chaguzi zimerudiwa, baada ya kufutwa.

“Chama hiki kina watu na wanachama wenye sifa nzuri kabisa za kuwa viongozi bora, wenye mioyo safi, wana ari kubwa ya kuwatumikia wananchi na wanachama, chama hiki kina watu wenye kila aina ya ujuzi na uwezo,”

“Lakini changamoto yetu ni baadhi ya wanachama kutengeneza miundombinu haramu ya kuwadhibiti watu wazuri wasipate dhamana za uongozi na waweke watu dhaifu kwa maslahi yao, hili chama tupo macho na tunafuatilia kwa karibu,” alisisitiza Katibu Mkuu.

Aidha, Katibu Mkuu Chongolo amewataka watendaji wa chama katika ngazi zote, kusimamia taratibu na kuweka mipango imara kuhakikisha mali na rasilimali za chama zinalindwa na kuziba mianya yote inayoweza kusababisha upotevu wake.

“Inasikitisha kuona mali ambazo chama inazimiliki kwa muda mrefu leo baadhi ya watu wanasubiri kuona zikipokonywa, tena wengine wanajitengenezea na uhalali… ili wazipore. Chama kitawachukulia hatua watendaji wote ambao watashindwa kusimamia na kulinda mali za chama hiki au kuacha tu zikipokonywa,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amewapongeza wanachama wote waliotumia haki yao ya kugombea na kuchaguliwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi na amewataka kuhakikisha wanazitumikia kikamilifu dhamana hizo.

Aidha, aliwataka watambue kuwa, kuaminiwa kwao ni ishara ya kubeba wajibu wa kuzidi kukijenga na kukiimarisha chama chao. “Mmepewa dhamana ya kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano, nendeni mkasimamie Ilani pamoja na miradi ya maendeleo kwa tija na kuhakikisha thamani ya fedha,”

“Hii itakisaidia chama kujiweka katika mazingira mazuri katika uchaguzi wa mwaka 2024 na 2025. Tuliomba dhamana ya kuongoza nchi. Tukisimamia vizuri Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kutatua changamoto za wananchi, hatutakuwa na maswali mwaka 2024 na 2025 bali tutakuwa na majibu.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here