Mwanaadamu ni taswira, kila akionacho ni cha muda na kidanganyifu

0

Na Mwandishi Wetu

FALSAFA inashajiisha kuuliza maswali mengi kuweza kuupata undani wa mambo. Lakini, katika ukweli wameweka vigezo vitatu. Cha kwanza ni elimu (Knowledge), maarifa au ujuzi wa jambo husika, cha pili ni uzoefu (Experiance), na cha tatu ni dhana iliyopo (Existing Concept) juu ya kitu au jambo hilo.  

Katika kitabu chake, ‘Archaeology: A Very Short Introduction,’ mtafiti wa mabaki ya kale Paul Bahn ameandika kuwa, ile hadithi inayodai kuwa mtu wa kwanza akiwa katika hali duni na asiyejitambua, aliibuka mamilioni ya miaka iliyopita imethibitika kielimu na kuzoefu kuwa haina ukweli.

Mwanaevolusheni Stephen J. Gould katika ‘Natural History,’ ameonesha kutilia shaka kubwa maelezo juu ya nasaba za masokwe wa kale wanaonasibishwa na wanaadamu kwa kuhoji nani anatokana na nani. 

Hatimaye akahitimisha kuwa utafiti wa wanasayansi wengi umeonesha kupingana kwa maelezo ya wanaevolusheni juu ya mtu anayedaiwa kuwa ndiye wa kwanza mwenye umbo la nyani ambapo wengine wanadai aliibuka miaka Milioni 2.3, wengine miaka Milioni 550, huku wengine wakidai miaka 30,000 iliyopita.

Hata hivyo, tafiti nyingine zinaonesha mifupa inayokadiriwa kuwa na miaka 20, 000 mpaka 27, 000 iliyopita si ya Mwanaadamu huyu wa sasa ingawa inafanana sana. 

Mwanasayansi Tim Bromage katika ‘New Scientific (1992)’ ameandika Sayansi na utafiti juu ya mambo ya kale umethibitisha kuwa, mabaki yaliyogunduliwa na kina Louise na Richard Leakey ingawa yanaelekea kufanana na Mwanaadamu huyu wa sasa, lakini silika na muundo wa mabaki hayo bila shaka ni ya viumbe wengine (Cro Magnon Men). Viumbe hao, hata hivyo, hawakuwa na utambuzi, uwezo wa kujitambua, akili wala elimu.

Wanasaikolojia wanaeleza ya kwamba, hata kama wanadamu wangalipewa umri mrefu zaidi, bado maisha ya ulimwengu huu yasinge wahakikishia furaha na starehe ya kudumu. 

Kwa mfano, miaka 80 mpaka 100 hivi leo, ndio umri mrefu ambao Mwanaadamu aliyejaaliwa kuufikia huitwa kikongwe. Katika umri huo, Wanasaikolojia wanaeleza ni kipindi cha utotoni tu cha kikongwe huyo, yaani tangu umri wa 0 hadi miaka 14 ambao pengine aliweza kuishi kwa furaha ya hapa na pale, ingawa pia wanakiri ni wachache mno wanaobahatika kuishi mazingira ya furaha.

Aidha, Wanasaikolojia wanaeleza lipo kundi la wachache zaidi kuanzia miaka 15 hadi 30 ambao wakati fulani hupata fursa ya kuishi kwa ‘furaha’. Hata hivyo, maana ya furaha hapa ni ile hali ya kuridhika, kutokuwa na hofu na kujihakikishia kupata mahitaji ya msingi ya mwanaadamu. 

Mitazamo mingine ya furaha ni ya kiuchumi zaidi kuliko kinafsi na kisaikolojia. Kwamba, wachache wenye furaha ni wale wanaoishi katika mazingira mazuri ya kiuchumi ambao hupata nafuu ya kula, kunywa na kulala pazuri pasi na kutingwa au kukabiliwa na majukumu mbali mbali ya kifamilia au kijamii. 

Wanasaikolojia wanasema, kwa kadiri maisha yalivyo, furaha itokanayo na uchumi mzuri hukatizwa na mitihani ya maradhi, ajali, kuuguliwa au kufiwa na ndugu au jamaa. Hali hii huelekea kwenye kubadili saikolojia ambapo badala ya furaha, ikageuka kuwa huzuni.

Inawezekana mtu wakati fulani akawa mwenye furaha ghafla akalazimika kuhuzunika. Pengine ni taarifa au tukio fulani ndilo lililokatisha furaha hiyo. Uzoefu unaonesha wakati fulani watu wa familia moja wanaweza kuwa kwenye furaha ghafla wakajikuta wakitawaliwa na majonzi au huzuni kutokana na labda msiba uliotokea katikati ya shangwe na hoi hoi inayoelezea furaha yao.

Miaka kabla ya 40, ni umri wa utu uzima wa katikati ambao huenda Mwanadamu huyu au yule aliweza kupata fursa ya kuishi kwenye hali na mazingira ambayo pengine yangesifiwa kuwa yalikuwa ya ‘furaha.’ 

Hata hivyo, kipindi chote kilichoendelea kufikia miaka yake 100, kwa waliobahatika kufika umri huo, bila shaka kilikuwa cha misongo, huzuni, adha, taabu, maradhi, wajibu na kuwajibika kwa ajili yake mwenyewe na/au kwa wengine.

Hatimaye Mwanaadamu huyo akamalizia umri huo unaoitwa ‘mrefu’ katika hali dhalili ya uzee. Umri huo dhalili ulimlazimisha kuwa duni na tegemezi wa kuhitaji msaada kwa kila jambo. Kwa ufupi Mwanaadamu huyu, katika uhai wake wote, ameishi muda mfupi sana wa furaha na muda ‘mrefu’ wa adha, taabu na huzuni. 

Kwa upande mwingine, kanuni za sayansi halisi za tangu na tangu pamoja na hatma ya vitu vyote sanjari na maarifa yahusianayo na maumbile, yanaonesha kuwa, upatanifu kati ya Mwanadamu na maumbile asilia umevurugwa, hali hiyo imesababisha matatizo makubwa zaidi katika maisha haya ya dunia. 

Kwa hakika hakuna jamii inayoweza kuwa na amani au furaha muda wa kuwa tabia za wanajamii wake zimekithiri kwenye uovu, shari na dhambi, hali inayoendelea sehemu mbali mbali duniani hivi sasa.

Haya ndiyo maisha, na huyo ndiye Mwanadamu aliyezungukwa ulimwenguni. Kwa ufahamu huu, akili ya kawaida ingefaa itusukume kuhoji kwa nini basi wawepo wachache sana wanaofikiri juu ya hili? 

Ulimwengu ni furushi la hisia?

Ulimwengu uonekanao, ni furushi la hisia, taswira na vivuli viundwavyo ubongoni mwa kila mtu. Taarifa zote zitokazo ‘Ulimwengu ulio nje’ ya mwanaadamu hukusanywa na milango mitano ya fahamu. 

Kuonekana kwa mawanda ya ulimwengu huu na malimwengu mengine, huwasilishwa ubongoni kupitia milango mitano ya fahamu. Macho hufanya kazi ya kuona, ngozi hufanya kazi ya kuhisi, pua hufanya kazi ya kunusa na kuvuta harufu, ndimi hufanya kazi ya kuonja na kutambulisha ladha na mwisho masikio nayo husikiliza sauti zote zinazopita hewani kwa njia mbali mbali. 

Kwa hiyo, ulimwengu ulio nje ya kila mwanaadamu ni ule unaotegemea taarifa za milango hii ya fahamu tangu kuzaliwa kwake. Hata hivyo, tafiti za kisayansi hivi leo, zimegundua mengi yanayoyatilia shaka yote yanayopokewa na milango mitano ya fahamu. Shaka hizo ni pamoja na je upo uhalisia wa Ulimwengu ambamo wanaadamu huishi? 

‘Ulimwengu ulio nje’ kwa mujibu wa tafiti hizo, ni taswira ambazo hujiunda ubongoni mwa kila mtu kama mwitikio wa ile mishtuo na michuruziko ya umeme ipitayo mwilini.

Wekundu wa tufaha, uyabisi wa mbao, umbile la mama, baba, familia au kile ambacho mtu anakimiliki kama nyumba, kazi na hata mistari ya kitabu hiki, ni athari ya mishtuo ya umeme ambayo ni tafsiri ya zile taarifa zipokewazo kupitia milango mitano ya fahamu na moja ya uungu.

Kuhusiana na hilo, Mwanasayansi Frederick Vester (1978) anaeleza ya kwamba, sayansi imefikia kuukubali ukweli kuwa mwanaadamu ni taswira na kila akionacho ni cha muda na kidanganyifu, na kwamba ulimwengu huu ni kivuli. 

Kuubainisha ukweli huu, hatuna budi kuchukuwa mfano wa mlango wa fahamu wa kuona, yaani macho ambayo kimaumbile ndiyo yenye nafasi kubwa ya kuusanifu ulimwengu ulio nje ya wanaadamu. 

Tendo la kuona lapatikana kupitia hatua endelevu kadhaa. Mkondo wa mwanga unaosafiri kutoka umbile fulani kwenda jichoni, hupita kwenye lenzi ambayo huuvunja vunja mwanga huo na kuutupa katika retina iliyo nyuma ya duara la jicho.

Kutokea hapo, mwanga ulio chini ya udhibiti maalumu, hugeuzwa kuwa ‘mawimbi umeme’ ambayo husafirishwa hadi kwenye  nyuroni ambayo nayo huupeleka mwanga huo mahala maalumu paitwapo ‘centre of vision’  sehemu ya nyuma ya ubongo yaani mahali panapofasiri mawimbi umeme kuwa taswira na kisha ‘vitu halisi’. 

Mawimbi umeme hugeuzwa taswira ubongoni baada ya mchakato mrefu unaofanyika kwa kasi kubwa. Kwa hakika, tendo hasa la kuona hufanyika katika sehemu hii ya ndani kabisa ya ubongo ambayo ni giza na iliyokingwa kabisa na mwanga.

Kwa hiyo, mtu anapodai kuwa ameona kitu fulani kilicho nje yake, kwa hakika alichokiona ni athari ya kile kilichofika mbonini kikageuzwa alama za ‘mawimbi umeme’ na kupelekwa ubongoni kisha kufasiriwa na kuundwa taswira. 

Hiyo ni kwamba, inaposemwa kitu fulani kimeonwa, kwa hakika kilichoonwa ni yale mawimbi umeme yaliyopewa taswira, si ule uhalisia wa nje wa kitu chenyewe kilichoonwa. 

Kwa hiyo, taswira zote zionekanazo kama vitu halisi, huundwa ubongoni mahala paitwapo ‘sehemu kuu ya ufasiri, uundaji na ufanyaji wa taswira’, yaani ‘center of vision’, eneo dogo sana kadiri ya sentimita chache ubongoni. 

Yale yote ambayo mtu huyaona au kuyatazama kwa macho yake, hupewa taswira kutoka kijieneo hicho kilichokingwa kabisa kuweza kufikiwa na mwanga, ni giza jeusi tii. 

Mfano wa mshumaa uwakao hupewa taswira na ubongo unaofanya kazi ya kupokea mwanga kutoka jichoni. Ubongo unaofanya kazi ya kufasiri haukutani moja kwa moja na mwanga asilia wa mshumaa huo. 

Wakati jicho linapokutana na mwanga wa mshumaa, ubongoni ni giza totoro. Ni kwenye sehemu hiyo ya ubongo yenye giza nene ambako ulimwengu hupewa taswira ya rangi mbali mbali zitokanazo na miali ya mwanga.

Kwa milango mingine ya fahamu utaratibu ni huo huo, ambapo sauti, hisia, ladha na harufu zote hufikishwa ubongoni na mawimbi umeme kisha kupewa taswira ya vitu halisi vyenye kuonwa, kushikwa, kuguswa, kuhisiwa, kunuswa, kuonjwa kusikiwa.

Kwa hiyo, katika michakato ambayo hatimaye hufasiriwa ama katika ‘kitovu cha taswira’ au katika ‘vitovu vya hisia’, ubongo unaofanya kazi zote zinazowasilishwa na milango ya fahamu haukutani moja kwa moja na maumbile asilia yaliyo nje ya Mwanaadamu.

Ubongo hufanya kazi ya kufasiri vivuli vinavyoundwa ndani yake. Ni kutokana na hili, ndio maana Mwanaadamu anaaswa asidanganyike na malimwengu yaundwayo ubongoni mwake. Kwa hiyo, kila kinachoonekana, kinachohisiwa, kuguswa, kusikiwa na kunuswa, kiwe maada, ulimwengu au malimwengu mengine, si chochote ila ni ‘alama umeme’ ziwasilishwazo ubongoni mwa wanaadamu kupitia milango ya fahamu. 

Kwa mfano, mtu anapokula tunda bivu, kwa hakika anachokutana nacho si lile tunda hasa bali ni hisia au athari ya taarifa ambazo milango ya fahamu hufikisha ubongoni. 

Kwa muktadha huo, umbile linaloitwa tunda kwa hakika ni kivuli kilichoundwa ubongoni kupitia mawimbi umeme ambayo huunda taswira, ladha, harufu na mguso unaoitwa tunda. Ndio maana nyuzi fahamu zinazosafirisha vivuli, zinapopatwa hitilafu ya ghafla, basi taswira ya tunda hilo nayo ghafla hutoweka.

Iwapo mawasiliano ya nyuzi fahamu yatakatwa, basi mchakato mzima wa harufu kwenda kwenye ubongo nao hukatwa hivyo kusababisha harufu kukoma kunusika ingawa tunda “litabaki kuwa na harufu yake ile ile” ambayo wengine wataendelea kuinusa na kuivuta!

Kwa hiyo, maisha ya ulimwengu huu ni ya taswira, hayana uhalisia kama ambavyo wengi hudhani. Kuuelewa ukweli huu ndiyo ufunguo wa kufahamu ya kwamba kuwapo kwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiko kwenye uhalisia.

Mtu anayeubaini ukweli huu hufahamikiwa kuwa kumbe maisha ya ulimwengu huu hayana uhalisia wa kumfanya mtu aishi atakavyo. Mwenye kuyafahamu hayo atatanabahi na kufikiri kwa kina yeye ni nani, katoka wapi, wapi alipo, anafanya nini na kwa lengo lipi na wapi aelekeako?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here