Na Dkt. Raymond Mgeni
BIASHARA huunganisha makundi mengi ya watu duniani na biashara imekuwako toka zama kale nyingi ambapo binadamu hakutumia pesa kupata mahitaji yake, bali kulifanyika biashara ya mabadilishano ya vitu toka pande mbili.
Mtu mmoja alileta ng’ombe na kubadilishana na mazao. Kadri zama zilivyozidi kubadilika, ndipo palipozaliwa mfumo mpya wa kufanya biashara ambao unatumia pesa.
Pesa ni thamani nyuma ya bidhaa au huduma inayotolewa katika mfumo mzima wa kibiashara unaogusia kuuza na kununua. Hivyo, watu wamekuwa wakikua kibiashara kwa pale ambapo wanazalisha faida nyingi zaidi kupitia kuuza bidhaa au huduma wanazotoa.
Hili limechangia wafanyabiashara kuhitaji mtaji zaidi ili wakuze biashara zao, ambapo hushawishika kuchukua mkopo iwe kwa kikundi fulani cha kifedha vya akiba na kukopa, Vikoba, vikundi vya kukopesha kwa riba, changizo za michezo pamoja na mabenki.
Mikopo imekuwa ikiwasaidia wengi kuwainua kibiashara pale ambapo inatumika kwa dhumuni hilo na mikopo pia imeleta madeni na taabu kwa watu wengi waliochukua kutoka katika vyanzo vinavyotoa pesa kwa riba na marejesho na kushindwa katika ulipaji.
Zipo sababu nyingi ambazo zinachangia watu wengi wanaochukua mikopo kushindwa kurejesha na wanaangukia katika madeni, kufilisiwa na kuanguka kibiashara na wakati huo wapo wengine kupata maradhi ya akili kama sonona na wengine kuthubutu kukatisha maisha yao kwa kuepuka madeni makubwa yaliyoleta malimbikizo ya riba na wakashindwa kulipa.
Mosi, kuchepusha au kutumia mkopo kwenda kwenye matumizi mengine yasiyo ya kiuzalishaji. Mkopo wa biashara kuingiza katika katika shughuli nje na biashara kumewaletea watu wengi taabu baadaye katika ulipaji. Kuchepusha mkopo ambao ungetumika kwa shughuli za uzalishaji ila mtu kutumia kwa ajili ya matumizi mengine ya kijamii kumesababisha matatizo mengi kwa watu.
Kuna mifano mingi ambayo watu waliochukua mikopo kutumia mikopo kwa ajili ya mambo ya kijamii kama kutumia pesa kwa matumizi ambayo hayakuwepo.
Hili huchangia katika marejesho kuwa magumu, maana mkopo ambao hautumiki katika uzalishaji unasababisha pasiwepo na faida na hilo linamfanya mtu ashindwe kurejesha na hatimaye kuelemewa na madeni.
Pili, biashara kwenda kinyume na matarajio. Kuna wakati ambao mtu hukopa kwa dhumuni jema, ila biashara inaweza kukumbana na changamoto ambazo zinasababisha pesa iliyokopwa kupotea na mtu kushindwa kurejesha fedha kwa wakati au kushindwa kabisa marejesho. Biashara hupanda na kushuka na inaweza kuathiriwa na vitu vingi vinavyoweza kuathiri uendeshaji wake.
Mtu hukopa akiwa na imani kuwa, kiasi cha pesa ambacho atakipata kitaisaidia biashara itanuke na kukua, ila kwenye biashara lolote linaweza kutokea. Mtu anaweza kuanzisha biashara ambayo ghafla inapoteza soko au kaingia hasara na kusababisha mzigo katika ulipaji wa fedha ya marejesho ambayo huwekwa katika riba.
Tatu, kuchukua mkopo mkubwa zaidi ya kile unachohitaji au mtaji. Kabla ya kuchukua mkopo ni muhimu kufahamu uwezo wako wa uwezekano wa kurejesha pesa utakayochukua na kile utakachoenda kufanyia shughuli za uzalishaji. Mkopo usiwe mkubwa zaidi ya mtaji ulionao ili isaidie pale ambapo utakopa na biashara isiende vizuri urejeshe pesa bila shida.
Ni hatari kwa mtu ambaye mtaji wa biashara yake ni Milioni 2 na anakopa Shilingi Milioni 10. Mikopo mikubwa imesababisha watu wengi waelemewe katika marejesho na kushindwa kabisa kulipa kutokana na wengine wanakopa mikopo mikubwa zaidi ya mitaji yao.
Nne, kubadili Mkopo na kuutumia kwa tamaa ya mambo mengine (starehe) ambayo si ya uzalishaji. Mkopo usipotumika inavyopaswa kutumika unaweza kugeuka madeni makubwa.
Madeni mengi ya watu waliokopa, imewatokea pale ambapo waliamua kutumia mkopo kwa starehe baada ya kuchukua na kuja kugutuka hawana kitu mfukoni na wana kazi ya marejesho yanayohitaji pesa iliyokopwa kwa riba.
Kutumia mkopo kwa anasa ni kutengeneza maisha magumu mbeleni kwa aliyekopa. Mkopo ni pesa ya kuogopwa na kuheshimiwa kama ilivyo ada ya shule. Unapojaribu kutumia kwa tamaa za maisha ya starehe, kununua vitu visivyoingiza pesa ni kujichimbia shimo la madeni.
Wengi waliojaribu kutumia mikopo kwa kutumia ovyo pesa kufanya starehe wameishia pabaya na hata kuwazuia kutokopeshwa tena wanapojulikana si watu wenye nidhamu na pesa ya mkopo.
Tano, kutumia mkopo kwa kufanyia biashara haramu au kinyume na sheria za nchi. Biashara zote ni muhimu kufanyika kutokana na mwongozo wa sheria za nchi ili kuepusha uendeshaji wa biashara kiujanja ujanja.
Biashara haramu ni pamoja na uuzaji wa biashara madawa ya kulevya, biashara za utoroshaji wa mali za Serikali kama viungo vya wanyama, utakatishaji wa pesa na kadhalika ambapo kunaweza kumtia mtu hatiani na kushitakiwa.
Lengo la mtu ambaye anachukua pesa ili kuendeleza biashara haramu kumesababisha watu wapoteze pesa, kukamatwa na kulipishwa faini na vifungo ambapo mtu hukosa nafasi ya kurejesha pesa alizokopa.
Sita, mkopo kupotea katika hali zisizotarajiwa mfano kupatwa na majanga; ugonjwa, kuibiwa, ajali za moto, ajali ziletazo ulemavu. Wakati mwingine mkopaji anaweza kupatwa na majanga mbalimbali yanayoweza yasizuilike kwa haraka kama kupata matatizo ya kiafya ambayo pesa aliyokopa ikaishia katika matibabu na ikawa changamoto kurejesha, kuna kuibiwa pesa, kupata ajali na kugharamika katika matibabu au kusababisha ulemavu mbalimbali unaoweza kuchangia ulegevu katika uzalishaji.
Hizi sababu sita ndizo zinazochangia marejesho ya mkopo yawe changamoto kwa watu wengi. Ni muhimu kuzingatia sababu zile ambazo mtu anaweza kuepuka mfano kutochepusha pesa ya mkopo kwa mambo mengine, kutotumia pesa ya mkopo kwa starehe kunaweza kumsaidia mtu ajiepushe kuingia katika matatizo ya hapa na pale ya ushindwaji wa kurejesha pesa aliyokopa.
0676 559 211
raymondpoet@yahoo.com