Na WAF-DODOMA
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema, ugonjwa wa Malaria bado ni changamoto Tanzania na unaipa mzigo mkubwa Serikali katika utoaji wa huduma za afya.
Waziri Ummy amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akifunga Mradi wa Okoa Maisha uliokua unatekelezwa katika Mikoa mbalimbali nchini hususan ile yenye maambukizi makubwa na kuzindua miradi miwili ya Shinda Malaria na Dhibiti Malaria inayofadhiliwa na Program ya Malaria ya Rais wa Marekani (PMI) unaogharimu Shilingi Bilioni 45 katika kipindi cha miaka minne.
Alisema, katika kipindi cha mwaka 2020 katika kila wagonjwa 100 waliolazwa kwenye vituo vya afya 16 ni wa Malaria, mwaka 2021 ni wagonjwa 13 na 2022 ni wagonjwa 12. Huku katika kipindi cha miaka mitatu, wagonjwa wa nje waliofika katika vituo vya kutolea huduma za afya kati ya 100 wagonjwa 10 wanakua wa Malaria.
Hata hivyo, Waziri Ummy alisema Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na Malaria ambapo imefanya vizuri katika kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na Malaria kutoka 6311 mwaka 2015 hadi kufikia 1905 mwaka 2021 sawa na asilimia 70.
Aidha, Waziri Ummy aliongeza kuwa, Idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Malaria katika vituo vya kutolea huduma za afya ilipungua kwa asilimia 23 kutoka Milioni 7.7 mwaka 2015 hadi Milioni 5.9 mwaka 2020. Huku kwa mwaka 2021, idadi ya wagonjwa wa malaria walikuwa milioni 4.4.
Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria ni mojawapo ya maeneo mengi ya afya ambayo Serikali imekuwa ikipokea ufadhili kutoka kwa watu wa Marekani. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2022 PMI imechangia zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 661 (sawa na Shilingi za Kitanzania Trilioni 1.55) kwa ajili ya Tanzania Bara na Visiwani kwenye mapambano dhidi ya malaria.
Vilevile, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi 2020, PMI imechangia zaidi ya asilimia 40 ya bajeti kwenye matibabu ya ugonjwa malaria nchini.