Na Saleh Ali
KILA mahali ngono imekithiri, mitaani usiseme, mashuleni ndio kabisa! Ngono ipo mabwenini, ngono ipo majumbani. Ushawishi wa kuingia katika uovu huu, ni mkubwa kwa vijana. Inaonekana kama vile vijana wanajitengenezea ulimwengu wao wa ngono na mapenzi.
Bila dini, ni kweli kimaumbile huwezi kuzuia utashi wa kinyama alionao binadamu katika tendo la ngono. Ni maumbile ya wanadamu kwa ujumla kwamba, wanaume huwatamani wanawake na wanawake huwatamani wanaume.
Hata hivyo, mahusiano ya kijinsia nje ya ndoa yameharamishwa. Suluhisho la pekee la kadhia ya uzinzi ni ndoa. Lakini, linapokuja suala la ngono kwa vijana, si kazi rahisi kuwashawishi kufunga ndoa kwa sababu nyingi.
Kwa vijana ambao wazazi wao hawana uwezo, na ambao hawana msaada wa kipato, hawana ajira wala kazi ya maana, suala la kufunga ndoa huwa ni muhali kwao. Na kwa wasichana ambao familia zao zina hali ngumu, na ambao hawana kazi wala biashara, tegemeo la maisha yao huwa ni maumbile yao.
Unaweza ukaona uhusiano hasi wa wanaume na wanawake ambapo upande mmoja unashindwa kuyaingia maisha ya ndoa kwa sababu ya uduni wa kipato, na upande wa pili unalazimika kutafuta kipato kwa njia isiyofaa.
Kwa kuwa vijana wa kiume wana fedha ya kuhonga tu na si ya kuolea, na kwa kuwa wasichana wanahitaji fedha ya kujikimu hata ile ya kuhongwa, moja kwa moja inajengeka jamii ya watu wanaokidhiana mahitaji ya kimaumbile na kibinadamu kwa njia isiyo rasmi.
Hii ndiyo hali inayoikabili jamii yetu hivi sasa. Kadri familia zinavyozidi kukabiliwa na umaskini, ndivyo jamii ya waasherati inavyozidi kustawi. Utafiti mitaani unaonesha kuwa, vijana wengi wanaishi maisha yasiyo rasmi, yakiwa kama vile ni majaribio ya ndoa.
Wanawekana kinyumba, lakini bila matarajio yoyote ya kuhalalisha unyumba wao. Kana kwamba kila mmoja anakaa mguu ndani, mguu nje! Mambo yakiwa magumu, hakuna sheria ya kuwabana ili kusaidiana kulea watoto.
Katika mazingira haya, mwanamke ndiyo anayebeba mzigo wote wa malezi pasipo msaada wa mzazi mwenziwe ambaye hakuna sheria ya kumbana kwani hakukuwa na mkataba wa ndoa.
Ndoa, kwa falsafa yake, ni kinga ya kimaumbile kwa mwanamama. Ndoa ina manufaa zaidi kwa mwanamke kwani inamfunga mwanaume atimize majukumu yake ya kifamilia. Maisha ya kuwekana kinyumba ni maisha yanayomweka mwanamke pagumu zaidi. Hana haki yoyote katika maisha haya.
Japo, wapo wanaodai kuwa mwanaume na mwanamke wakiishi kwa muda mrefu ndio tayari wameshakuwa mume na mke, lakini hakuna ushahidi wa kimaandishi wa kumsaidia mwanamke kupata haki zake kama anavyozipata katika ndoa.
Kwa ajili ya kutafuta nafuu ya mzigo wa gharama, wasichana wadogo huamua kujenga mahusiano na wanaume watu wazima wakiamini kuwa hawa hawatawakimbia, bali watawalea wao na watoto wao.
Wanaamini kuwa, wanaume wakubwa huwa watulivu zaidi kuliko ‘vivulana’ ambavyo haviishi tamaa ya kubadili wanawake. Haishangazi hivi leo kumkuta binti wa miaka 18 akimtaka baba wa miaka 40 na kuendelea!
Matokeo ya ongezeko la maisha ya kuwekana kinyumba miongoni mwa vijana hivi leo ni ongezeko la watoto wa mitaani ambao sasa wanahalalishwa kwa jina la Soka.
Mtu anashindwa kuelewa kama ni fahari au fedheha kwa Taifa kutwaa ubingwa wa soka wa dunia katika mashindano ya timu za watoto wa mitaani. Kwamba, kupitia ubingwa huo, Tanzania sasa ni maarufu duniani kwa watoto wa mitaani!
Hii inazidi kuchochea hisia kuwa kumbe kutelekeza watoto kuna tija, na hivyo watu waendelee kuzini ili kuendelea kudumisha timu za watoto wa mitaani. Kuwa na watoto wa mitaani ni matusi kuwa Taifa limeshindwa kuziwezesha familia kulea watoto, au familia za Watanzania zimeshindwa kulea watoto!
Lakini, kimsingi ni matokeo ya mfumo wa jamii ambapo mahusiano ya wanaume na wanawake hayarasimishwi. Ni kweli ipo migogoro ya wanandoa inayosambaratisha familia, lakini wastani wa watoto wa mitaani wanaotokana na migogoro hiyo si mkubwa sana. Watoto wengi wa mitaani ni wale wanaozaliwa nje ya ndoa.
WANAFUNZI NA NGONO
Kama yalivyo mazingira ya mitaani, mazingira ya shule nayo si salama. Matarajio ya wazazi na wanafunzi wenyewe wakati mwingine hushindwa kutimizwa kwa sababu za kimazingira.
Mzazi alikusanya nguvu zake kumsomesha mtoto kwa matarajio kuwa atafika mbali kielimu, na mtoto naye alianza vema masomo kwa matarajio kuwa safari yake ya elimu itafika mbali, lakini ghafla anakutana na mazingira ya kumtoa kwenye ajenda ya masomo na kushika mambo mengine. Watoto wengi wamedondoka na kufadhaisha wazazi wao.
Wengine hukwama hata kabla ya kuanza masomo. Kujiingiza katika mambo yasiyofaa ndiko kunakozuzua akili yao hata wasione maana ya kuendelea na masomo wakiamini kuwa yale wanayoyataka watayapata vizuri kwa kukataa kusoma.
Utafiti wa Kimataifa unaonesha kuwa, mwanafunzi katika nchi za Magharibi humaliza kidato cha juu cha elimu akiwa na umri wa miaka 18. Kwa wastani hupitisha miaka minne ya masomo kabla ya kupata shahada ya kwanza.
Labda sasa kada za elimu zifikiri namna ya kuipunguza safari ya masomo bila kupunguza ubora wa elimu. Elimu iwe bora zaidi kiasi kwamba darasa la tano liwe kikomo cha elimu ya msingi.
Wengine wakafikiria njia mbili mbadala za kuhakikisha kuwa wasichana wanaendelea na masomo. Wapo wanaosema kuwa wasichana wanaopata mimba waendelee na masomo baada ya kujifungua.
Wazo hili likapata upinzani wa hoja kuwa kuwaruhusu wazazi shuleni ni kufungua kliniki ya wajawazito kwani hiyo itawahamasisha watoto wote wa kike kuzini bila hofu. Angalau hofu ya kufukuzwa shule huwafanya wengi wao wajichunge.
Wengine wakatoa wazo kuwa waolewe na kisha waendelee na masomo. Lakini, mtafiti mmoja anasema kuwa punde unapokuwa na watoto wawili na kisha ukalazimika kufanya kazi muda wote kuikimu familia yako, utaweza kuwa na muda na nguvu za kwenda shule? Ni vigumu na ni hatari kwa familia pale mke anapojitoa kwa ajili ya masomo.
Zinaa imehalalishwa kwa njia nyingi. Wapo wanaoona kuwa mipira ya zinaa inaweza kumuhakikishia binti ngono salama ili amalize masomo yake. Kwa mtazamo wa kijahili, hiyo yawezekana, lakini zinaa ni dhambi, haitazamwi kama kizuizi tu cha masomo, bali inatazamwa kama uasi kwa Mwenyezi Mungu.
Kumuasi Mungu kwa njia ya mpira hakukubaliki. Muhimu ni kuwafundisha vijana wetu kujizuia uovu wa zinaa; subira au kuoa na kuolewa. Ipo hali ya kujiamini kwa baadhi ya wazazi kuwa watoto wao wako salama, hawajihusishi na mambo yasiyohusiana na masomo yao.
Wanaamini kuwa hawawezi na hawataweza kufanya mambo ya kipuuzi. Hapana! Wasijiamini mno na wasiwe na shaka mno. Wabakie kati kwa kati huku wakichukua tahadhari zote. Wazazi wasielezee zinaa kwa watoto wao kwa sura ya tishio la masomo au UKIMWI.
Kama hoja ya kumtaka mtoto aepuke zinaa ni mimba itakayomfukuzisha shule au UKIMWI, naye anaweza kujenga hoja akilini kuwa kama atatumia njia salama ya kumkinga na mimba na UKIMWI, ni ruhusa kwake kuzini? Hapa hatutatui tatizo, bali tunaipa nguvu zinaa salama!
Kama tumeshindwa kufundisha imani ya kuwawezesha wanafunzi kufanya subira, basi tufikirie njia ya ndoa. Na hoja ya kupunguza umri wa kukaa shuleni inaweza pia ikasaidia. Kwamba, baada ya miaka mitano ya elimu ya msingi, mtoto apande ngazi badala ya kuendelea na darasa sita na la saba ambayo hayabadilishi chochote katika msingi wa elimu ya sekondari.
Tunaweza kumpunguzia safari ya shule, na muda wa kusubiri. Kama mathalani atamaliza kidato cha sita akiwa na miaka 18, angalau hadi miaka 22, atakuwa amemaliza shahada. Sasa ana muda wa kuolewa mapema. Kuharakisha ndoa ni jambo muhimu zaidi kimaumbile.