Kamati ya bunge ya Bajeti yaridhishwa na ushushaji na upimaji wa mafuta Bandarini

0

Na Mwandishi Wetu


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imefanya ziara katika maeneo yanayotumika kupakua mafuta kutoka kwenye Meli na kupima katika Bandari ya Dar es Salaam na Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kujihakikishia kuwa, kazi za ushushaji wa mafuta na upimaji mafuta katika sehemu hizo zinafanyika kwa ufanisi na Serikali inapata mapato stahiki.

Baada ya kufanya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Daniel Sillo, aliipongeza Serikali kwa jinsi ilivyowekeza katika miundombinu ya ushushaji wa mafuta pamoja na mita za kupimia mafuta hayo ambazo kwa miaka ya nyuma zilikuwa hazipo na hivyo Serikali ilikuwa haipati mapato stahiki.

Alisema kuwa, mita hizo za kupimia mafuta licha ya kuiwezesha Serikali kupata mapato inayostahili,  kampuni zinazoagiza mafuta hayo kutoka nje ya nchi pia zinapata uhakika wa kiasi cha mafuta ambacho wamekiagiza.

Vilevile alisema, Kamati hiyo ilifanya ziara  katika Bandari ya Mtwara ambapo pia Wajumbe walishuhudia juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuiendesha sekta ya mafuta kwa ufanisi kwani mita za kupimia mafuta katika bandari hiyo zinafanya kazi vizuri na pia upanuzi wa bandari pamoja na sehemu za kuhifadhia mafuta unaendelea vizuri hali itakayofanya bandari hiyo kupokea mafuta kwa wingi zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here