Mapinduzi ndani ya vyama,
ni hadithi ya kusisimua

0

Na Mwandishi Wetu

KWA miaka 30 baada ya Vyama vingi kuruhusiwa tena kwa mujibu wa sheria Namba 5 ya mwaka 1992 baada ya mfumo huo kufutwa mwaka 1965, kumekuwa na mfululizo wa Mapinduzi kadhaa yaliyotokea ndani ya baadhi ya vyama vya siasa nchini.

Kutokea kwa Mapinduzi hayo kumekifanya Chama tawala CCM kipate mwanya wa kuwaeleza wananchi kuwa, viongozi wa vyama hivyo hawana uwezo wowote wa kujenga taasisi makini, bali ni waganga njaa na wenyewe ubabaishaji mwingi.

Kwa vyovyote maneno hayo yalioonekana kuwaingia mioyoni na akilini baadhi ya wananchi wanaoendelea kuamini na kusema ama kwa hakika vyama hivyo vinaisindikiza CCM ibaki madarakani.

Mapinduzi ya kwanza ni pale alipong’olewa Chifu Abdalahh Said Fundikira wa UMD katika kiti chake cha Uenyekiti huku akiwa muasisi wa chama hicho.

Kundi liliongozwa na Simon Kashura baada ya kuzuka mtafaruku katika ya Chifu Fundikira na Katibu Mkuu wake Christopher Kasanga Tumbo.

Kashura naye awali alishiriki njama zilizomng’oa madarakani Wilfred Mwakitwange wa chama cha PONA ambacho sasa kimefutwa kisheria akiwa na mshirika wake Peter Terry.

Upepo wa ‘mapinduzi’ ukahamia CUF baada ya Mwenyekiti muasisi James Mapalala kuondoshwa na kundi la wana CUF walioongozwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake Maalim Seif Sharif Hamad.

Mvutano kati ya kundi la vigogo hao wawili ulidumu kwa miezi kadhaa, hatimaye ukaamuliwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CUF mbele ya Msajili wa vyama vya siasa Jaji George Liundi.

Hatua hiyo ikampa nafasi Waziri wa zamani wa Ardhi na Makazi katika Serikali ya Awamu ya Kwanza Mageni Musobi Mageni kushika haramu Uenyekiti mpya wa CUF kabla ya Profesa Ibrahim Lipumba.

Mgogoro mkubwa ukaibuka NCCR – MAGEUZI na kukigawa chama hicho katika makundi mawili makubwa. Kundi moja liliongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wake Augustino Mrema na kundi jingine la Katibu Mkuu wake Mabere Marando.

Mrema alijiunga na NCCR – MAGEUZI baada ya kujiondoa CCM kutoka na lililoitwa sakata la mashamba ya Chavda na kukamatwa kwa dhahabu katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa, jijini Dar es Salaam.

Hatua ya kutokea kwa ugomvi huo ikalifanya kundi la Mrema aliyekuwa akiungwa mkono na wanasiasa akina Prince Bagenda, Mustafa Wandwi, Cosmas Chenyenge waliungana na Mrema walipotimuliwa NCCR – MAGEUZI na kuhamia TLP.

Kundi la Marando ambalo lilikuwa na wanasiasa vijana na wasomi akina Monase Nyambabe, Idris Al Noor, Joseph Selasini, Dkt. Ringo Tenga, Anthony Komu, na Masumbuko Lamwai wakabaki NCCR – MAGEUZI chini ya uongozi wa Marando.

‘Jua halikuchwa’ ila Mapinduzi mengine ya ‘kimkakati’ yalitokea ambayo yaliongozwa na James Mbatia na baadhi ya wenzake waliomuondoa Kiongozi muasisi wa chama hicho Marando na kumuweka nje ya uzio kupitia Uchaguzi Mkuu uliojaa hila na mizengwe.

Hekaheka za kuondoana Kimapinduzi zikaelekea TADEA, wakati huo kabla ya hakijajulikana kwa jina ADA – Tadea kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wake muasisi Oscar Kambona.

Mwanasiasa wa siku nyingi Dunstun Liffa Chipaka akatwaa madaraka kutokana na uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho na kujitangaza yeye ndiye rais mpya wa Tadea.

Ndani ya TLP hali ya maelewano ikavurugika kati ya Mwenyekiti wa Chama hicho Leo Lekwama kuvutana na Katibu Mkuu wake Seneta Julius Miselya hatua iliyokifanya chama hicho kipoteze amana yake kisiasa kwa jamii.

Lwekamwa baada ya kufungua milango na kulikaribisha kundi lililojitoa NCCR – MAGEUZI chini ya Mrema naye hakudumu, kwani alijikuta akisombwa na upepo wa Mapinduzi.

Bundi wa Mapinduzi akatua juu ya paa la nyumba ya UDP chini ya uongozi wa John Momose Cheyo alipoondolewa madarakani na kundi la wanasiasa ‘shababi’ wakiongozwa na akina Amani Nzugile Jidulamabambas, Erasto Tumbo, Danny Makanga na Hamad Yusuf.

Hata hivyo, wakati aliyekuwa Msajili wa vyama vya siasa George Liundi akayatambua mapinduzi hayo, ujio wa Msajili aliyekalia kiti baada ya Liundi, John Tendwa akabatilisha Mapinduzi hayo na kuurudisha utawala wa Cheyo.

Joto la kutaka mabadiliko ya demokrasia likaonekana kutanda ndani ya CHADEMA kufuatia madai ya kuwepo uongozi wa muda mrefu wa Mwenyekiti wake muasisi Edwin Mtei na Katibu Mkuu wake Bob Nyange Makani kutakiwa kuondoka.

Hatua hiyo ikawalazimisha vigogo hao kuamua kukaa pembeni mapema ili wasikipasue chama hicho na kufanikiwa kukinusuru baada ya kuridhia kujiweka kando. Freeman Mbowe akashika usukani huku Amani Warid Kaborou akiwa Katibu Mkuu.

Kabla ya vigogo hao kukaa kwao pembeni, baadhi ya wanasiasa waliamua kujiondoa na kuanzisha chama akiwemo Jockob Nkomola ambaye baadae alihamia CCM.

Kufanyika kwa uchaguzi mkuu uliomuweka kando Mosobi Mageni wa CUF, kunampa upenyo Profesa Ibrahim Lipumba awe Mwenyekiti mrithi, huku aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Maalim Seif kuwa Katibu Mkuu na Katibu Mkuu muasisi, Shaaban Khamis Mloo alipoachana na siasa.

Maalim Seif na Lipumba hawakuiva chungu kimoja, kwani maelewano kati yao yakawatenganisha na kuzuka mgogoro mkubwa ambao ulizitikisa siasa za chama hicho na kukipasua.

Mtafaruku huo ulikwenda sanjari na kujitoa kwa baadhi ya wanachama akiwemo mwanasiasa wa siku nyingi na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa fedha katika Serikali ya Awamu ya Kwanza Hamad Rashid Mohammed akiwa na Said Miraj Abdullah walioanzisha ADC.

Kama Mbatia alivyoshiriki njama za kumuondoa Marando ndani ya NCCR – MAGEUZI ndivyo inavyoonekana sasa jinsi kundi jingine jipya la Joseph Selasini lilivyomng’oa Mbatia kama kina Marando na Mbatia walivyomuondoa Mrema ambaye naye akawapoka chama akina Lekamwa TLP.

Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, ukianza kula nyama ya binadamu hutaacha, pia wahenga wa kale wakasema, ukipindua jiandae kupinduliwa, lakini ikiwa kwa ncha ya upanga jiandae kufa kwa upanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here