Serikali yaidhinisha Bilioni 150 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea 2022/2023

0

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema, Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha Shilingi Bilioni 150 kutumika kwa ajili ya ruzuku ya mbolea ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa wingi na kwa gharama nafuu.                                              

Majaliwa alisema, katika msimu wa 2022/2023, utoaji wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima unalenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini na hivyo kuwa na usalama wa chakula na kukidhi upatikanaji wa malighafi za viwanda vya ndani.

Waziri Mkuu alisema, wakati akiahirisha mkutano wa nane wa Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma. Alisema, Rais Samia anatambua umuhimu wa pembejeo katika kuongeza tija kwenye kilimo.

Alisema, hadi kufikia Agosti 31, 2022 wakulima 956,920 wamesajiliwa kwa ajili ya kupata mbolea ya ruzuku ambapo jumla ya tani 60,882 za mbolea zimenunuliwa na wakulima katika mikoa ya Arusha, Iringa, Mbeya, Morogoro, Njombe, Rukwa, Ruvuma na Songwe. “Nitumie fursa hii kuilekeza Wizara ya Kilimo kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kwa wakati.”

Waziri Mkuu alisema, katika kipindi cha mwaka 2021/2022, tathmini awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula imeonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula umefikia tani Milioni 17.4, ambapo kati yake uzalishaji wa mazao ya nafaka ni tani Milioni 9.4 na mazao yasiyo ya nafaka ni tani Milioni 7.9.

“Mahitaji yote ya chakula yanayojumuisha nafaka na yasiyo ya nafaka kwa mwaka 2022/2023 ni zaidi ya tani Milioni 15 ambapo tani Milioni 9.5 ni za mazao ya nafaka na tani Milioni 5.5 ni mazao yasiyo ya nafaka. Kwa kulinganisha uzalishaji na mahitaji, nchi yetu ina kiwango cha utoshelevu wa chakula wa asilimia 115.”

Alisema, ili kuhakikisha hali ya chakula nchini inaendelea kuimarika, Serikali imeuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kuhifadhi tani 147,142 na kuendelea kununua mazao ya chakula kwa ajili ya kuhifadhi. “Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuhifadhi akiba ya chakula tuliyonayo na kuwa na matumizi sahihi ya chakula.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema maandalizi ya msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 yanaendelea sambamba na kuwezesha upatikanaji wa pembejeo muhimu hususani mbolea.

“Wastani wa matumizi ya mbolea nchini katika kipindi cha kati ya mwaka 2019/2020 hadi 2021/2022 umeendelea kuwa tani 430,000. Hadi kufikia Agosti 31, 2022 upatikanaji wa mbolea nchini umefikia tani 213,403 sawa na asilimia 49.6 ya wastani wa matumizi ya mbolea.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here