Diplomasia ya uchumi itilie mkazo masoko ya bidhaa za Tanzania

0

Na Hussein Chimba

WAKULIMA wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara pamoja na wazalishaji wa bidhaa za viwandani, wana nafasi kubwa ya kuongeza mauzo yao na hatimaye kuwa mamilionea kama suala la masoko ya uhakika litafanyiwa kazi kikamilifu.

Uzalishaji wa bidhaa za kilimo na za viwandani bila uwepo wa masoko ya uhakika ni hasara tupu kwa wazalishaji.

Zaidi ya asilimia 70 ya watanzania ni wakulima na kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu. Hakuna namna ambayo wakulima wa wawekezaji wa viwanda wanaweza kubadili maisha yao kwa kupata faida ya jasho lao kama masoko ya bidhaa zao yatakuwa ya kusuasua.

Hivyo, katika jitihada za kumkwamua mkulima mdogo wa Tanzania na wawekezaji wa viwanda, ni vyema kuweka mazingira bora ambayo watauza mazao yao kwa bei nzuri inayoendana na uwekezaji wa nguvu na mitaji yao kwenye kiilimo na viwanda.

Jitihada za ukuzaji uchumi katika Mataifa mbalimbali duniani yanachagizwa na ‘Diplomasia ya Uchumi,’ ambayo inakuza ushirikiano wa baina ya nchi moja na nyingine.

Diplomasia ya uchumi ni ushirikiano kati ya nchi moja na nyingine katika ukuzaji wa uchumi kwa maslahi ya nchi zinazoshirikiana (Win win situation). Ni jambo la faraja kuona Tanzania nayo haiko nyuma, bali inaitumia vizuri diplomasia ya uchumi katika maendeleo ya viwanda na ukuzaji wa uchumi.

Kwenye hotuba yake wakati wa kulihutubia bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dodoma, 22 Aprili 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alisema, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kutekeleza shughuli za Kidiplomasia kuendana na Sera ya Diplomasia ya Uchumi na kuahidi kuimarisha na kukuza Uhusiano na Mataifa mengine pamoja na Jumuiya za kikanda na Taasisi za Kimataifa.

“Ili kutimiza azma hiyo, tunakusudia kuimarisha utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Balozi zetu zilizoko nchi mbali mbali duniani, kwa kuajiri watumishi wenye sifa na weledi wa kazi na kusambaza vitendea kazi, pamoja na kutumia kiuchumi majengo na viwanja ambavyo ni mali ya Tanzania vilivyoko nje ya nchi.”

“Kwa madhumuni ya kuwezesha utekelezaji mzuri wa Diplomasia ya Uchumi, tutafungua na kuanzisha pia Balozi mpya, Konseli pamoja na Vituo vya Biashara kwenye nchi na miji ya kimkakati ili kutangaza vivutio vyetu vya utalii, kuvutia uwekezaji na kutafuta masoko ya bidhaa zetu. Tutafanya uchambuzi wa kitaalamu utakaobaini nafasi ya kila ofisi ya ubalozi katika kukuza biashara, uwekezaji na utalii. Uchambuzi huo ndio utatumika kupanga maafisa kulingana na uwezo wa kila Ubalozi,” alisema Rais Samia.

Zipo Jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali za kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta mbalimbali hasa kilimo, viwanda na huduma nyingine za kijamii. Jitihada hizi zimezaa matunda, kwani wawekezaji wengi wamevutiwa kuwekeza Tanzania na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wetu.

Lipo eneo jingine la upatikanaji wa masoko kwa mazao na bidhaa kutoka Tanzania, ambapo jitihada za makusudi zinapaswa kuongezwa ili kusaidia maendeleo ya kilimo, viwanda na ukuaji wa uchumi. Viongozi wa Serikali na watanzania wengine wasiishie kuonyesha tu maeneo ya uwekezaji Tanzania, bali pia watangaze mazao na bidhaa zinazozalishwa Tanzania ili kupata soko la uhakika na kuongeza uzalishaji.

Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi ya kutosha na nzuri yenye rutuba ambayo mazao ya chakula na biashara huzalishwa kwa wingi. Mazao kama mahindi, ufuta, alizeti, maharagwe, mbaazi, mawese, matunda ya aina mbalimbali, mbogamboga, viazi, chai, katani, kahawa, korosho, pamba nk, huzalishwa kwa wingi.

Viwanda vyetu zinazalisha bidhaa bora kabisa zenye kumudu ushindani katika masoko ya Kitaifa na Kimataifa. Mazao yote haya yanahitaji masoko ya uhakika ili wakulima waweze kufaidi jasho na mitaji yao waliyowekeza katika uzalishaji.

Ni wakati wa balozi zetu zilizopo katika nchi mbalimbali kutangaza na kutafuta masoko ya mazao na bidhaa zinazozalishwa Tanzania. Mabalozi wetu wawe kiungo wa kuunganisha wakulima na wazalishaji wa Tanzania na wanunuzi waliopo katika nchi wanazoiwakilisha Tanzania ili upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao na bidhaa za Tanzania liwe jambo halisi.

Kila balozi awe na deni la kuhakikisha anafanya kitu kwa ajili ya wakulima wa Tanzania na kwa wawekezaji wanaozalisha bidhaa kutoka Tanzania ili kuboresha hali zao za maisha na kukuza uchumi wa nchi. Bidhaa na mazao yanayozalishwa nchini yanahitajika sana katika nchi mbalimbali duniani, lakini tatizo limekuwa ni ukosefu wa watu kuyachangamkia masoko hayo. Ulimwengu wa sasa ni wa ushindani katika kila jambo, Watanzania hatupaswi kujifungia kusubiri masoko yatutafute bali sisi kuyatafuta masoko hayo na kupeleka bidhaa zetu.

Mkulima wa kijijini kabisa kumwambia changamkia soko la mbaazi nchini India ni kumchanganya zaidi, kwani atashindwa kujua aanzie wapi, aishie wapi kuiuza mbaazi yake. Lakini, Serikali kupitia balozi zetu zitakapoandaa utaratibu mzuri wa namna ya wakulima watakavyoiuza mbaazi yao India, itakuwa rahisi kwa wakulima kufanya hivyo. Mabalozi wetu wanaandae mikutano ya kuonana na wafanyabiashara na wanunuzi wa mazao na bidhaa ili kutangaza fursa za mazao na bidhaa kutoka Tanzania.

Hakuna sababu ya Tanzania kuwa watazamaji wa masoko ya uhakika yaliyopo nje ya nchi wakati mahitaji hayo yanapatikana Tanzania na kwa kiwango kikubwa. Diplomasia ya uchumi itumike kikamilifu katika kubadili maisha ya wakulima. Jambo la kuzingatia ni wakulima wetu kuzalisha mazao na bidhaa zilizo katika ubora unaokidhi viwango vya Kimataifa ili kuwavutia wanunuzi.

Tanzania ya viwanda na ya uchumi wa kati juu na baadaye uchumi wa juu inawezekana kama diplomasia ya uchumi itajikita katika utafutaji wa masoko ili kuwasaidia wakulima wetu kutolanguliwa na wafanyabiashara wasio waaminifu wanaonunua mazao kwa bei ndogo yenye kuwatia hasara wakulima wetu.

Mwandishi wa makala hii ni mbobezi na mchambuzi wa masuala ya elimu, uongozi na utawala na pia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkwala iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Kongwa jijini Dodoma. Anapatikana kwa namba: 0764 091 917.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here