Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amesema Serikali itatoa kila aina ya msaada kuhakikisha Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Dkt. Mwinyi alisema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Camillus Mongoso Wambura, ambapo pamoja na mambo mengine amefika kwa ajili ya kujitambulisha.
Alisema, Serikali inatambua uwepo wa changamoto mbali mbali zinazolikabili Jeshi hilo, hivyo akabainisha azma ya Serikali katika kuzitafutia ufumbuzi ili kuliwezesha jeshi hilo kutekeleza vyema majukumu yake.
Alisema, lengo la kuwepo vyombo mbali mbali vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Polisi ni kuhakikisha kunakuwepo usalama wa kutosha hapa nchini, huku akibainisha ushirikiano kuwa ndio kichocheo cha kuleta ufanisi wa vyombo hivyo.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kuwa, Serikali inaridhishwa na utendaji kazi wa Jeshi hilo na hivyo akasisitizaazma ya kuendeleza ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jeshi hilo.
Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza IGP Wambura kwa uteuzi aliopata katika chombo hicho kikubwa na chenye umuhimu mkubwa katika usalama wa nchi.
Nae, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Camillus Mongoso Wambura alisema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, imekuwa katika juhudi kubwa ya kuipatia ufumbuzi changamoto ya upungufu wa vifaa na vitendea kazi muhimu vya Jeshi hilo, hususan katika nyanja ya usafiri.
Alisema pamoja na Serikali kutoa fedha za kutosha kwa Jeshi hilo kwa jili ya ununuzi wa Vifaa, lakini hivi karibuni imepokea msaada mkubwa wa magari 72, huku magari mengine 78 yakiwa njiani (katika meli) kuja nchini.
“Kuna magari mengine 117 yanaendelea na matengenezo kiwandani kwa ajili ya Jeshi letu na mara tu yatakakamilika yataletwa hapa nchini”, alisema.
IGP Wambura alisema, ugavi wa magari hayo tayari umefanyika, ambapo Jeshi la Polisi Zanzibar limepatiwa jumla ya magari kumi (10) kwa ajili ya Mikoa Mitano, Chuo cha Polisi Ziwani pamoja na Kikosi cha kutuliza ghasia ‘Field Force Unit’.
Aidha, alisema Mikoa hiyo pamoja na Mikoa mingine ya Tanzania Bara itaendelea kupatiwa magari hayo kadri yatakavyowasili hapa nchini.
Akigusia suala la kukosekana kwa usalama katika mipaka ya Zanzibar, IGP Wambura alisema, kwa kuitikia agizo za Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na Usalama ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu, Jeshi hilo linalifanyika kazi kikamilifu suala hilo kwa kuzingatia umuhimu wa usalama nchini.
Alisema, kwa kuanzia wamefanya kikao muhimu kilichowashirikisha Maofisa wa Jeshi hilo kutoka pande mbili za Muungano ili kubaini chanzo cha tatizo hilo pamoja na kuzingatia uwepo wa rasilimali watu kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.