Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais Deogratius Ndejembi, amesema, fedha za Serikali zilizotengwa kwa ajili ya vijana ni lazima ziwafikie walengwa na kuleta matokeo yanayopimika kiuchumi.
Ndejembi alitoa kauli hiyo Novemba 23, 2026 wakati akizungumza katika hafla ya kuwasilisha mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha pili kwenye sekta ya maendeleo ya vijana, iliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais ameliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kusimamia mchakato wa kuunganisha mifuko na programu 75 za uwezeshaji kuwa mfuko mmoja utakaorahisisha upatikanaji wa mitaji na dhamana kwa wananchi, hususan vijana.
Alisema, hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto zinazowakabili vijana wengi wanaoshindwa kupata mikopo katika taasisi za fedha kutokana na kutokuwa na dhamana zinazohitajika.
Akizungumzia fedha zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana, Ndejembi alisema, Shilingi Bilioni 200 zinapaswa kutolewa kwa haki na bila upendeleo ili kuwafikia vijana wa mijini na vijijini, wakiwemo vijana wenye ulemavu.
Aliwataka wasimamizi wa fedha hizo kuhakikisha hazitumiki kulipia posho za watumishi au kununulia magari, bali kuelekezwa katika shughuli zinazozalisha mitaji, biashara na ajira.
Pia, alisisitiza kuwa, mafanikio ya uwekezaji huo hayatapimwa kwa kiasi cha fedha kilichotolewa pekee, bali kwa idadi ya biashara zilizoanzishwa, zilizokua na ajira zilizozalishwa.
Aidha, alizitaka Wizara, taasisi za umma na halmashauri kuhakikisha vijana wanaotekeleza zabuni za Serikali wanalipwa kwa wakati ili kuepusha changamoto za mtaji zinazoweza kudhoofisha biashara zao.
Akieleza ukubwa wa changamoto ya ajira nchini, Makamu wa Rais alisema takribani vijana 900,000 huingia katika soko la ajira kila mwaka, lakini karibu mmoja kati ya vijana kumi pekee ndiye anayepata ajira rasmi.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, alisema taasisi za umma zimeahidi kutoa takribani nafasi 600 za mafunzo kwa vitendo, huku Serikali ikiwa na malengo ya kufikisha nafasi 10,000 katika mashirika ya umma na 20,000 katika sekta binafsi.
Ndejembi aliwahimiza vijana kutumia fursa zinazojitokeza, kuendelea kujifunza na kubuni njia mpya za kujiajiri badala ya kusubiri ajira za kuajiriwa pekee.
Katika hatua nyingine alisema, AFCON 2027 itakayofanyika Tanzania, Kenya na Uganda kuwa fursa muhimu kwa vijana kujipatia ajira na kipato kupitia huduma mbalimbali zitakazohitajika wakati wa mashindano hayo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Arthur Nanauka, alisema, Serikali imeendelea kutekeleza mipango ya uwezeshaji vijana, ambapo hadi sasa Shilingi Bilioni 52.69, sawa na asilimia 26 ya fedha za mpango wa Shilingi Bilioni 200, zimepelekwa katika wizara zinazohusika na utekelezaji wa mpango huo.
Alisema, mpango huo pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umechangia kuzalisha ajira 44,615 kupitia miradi 3,950 katika mwaka wa fedha unaoendelea.
Nanauka ameeleza kuwa, mikopo inayotolewa kupitia Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana haina riba, huku muda wa kuanza kurejesha ukizingatia mzunguko wa uzalishaji wa shughuli zinazofadhiliwa.
Akitoa mfano wa matokeo ya uwezeshaji huo, ametaja kijana Imani Mpinga, mkulima wa alizeti aliyepata Shilingi Milioni 263 kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kusafisha mafuta ya alizeti katika Kijiji cha Makunda, ambacho tayari kimeanza kuuza bidhaa zake.
Katika eneo la ununuzi wa umma, Waziri huyo alisema, vikundi vya vijana vimepata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 12.99, huku Serikali ikiwa na lengo la kufikisha thamani ya zabuni hizo Shilingi Bilioni 50 kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha.
Aidha, alisema takribani vijana 400,000 wamejisajili katika mfumo wa Kidijitali wa Youth Empowerment System (YES), unaolenga kuwaunganisha vijana na taarifa za ajira, mitaji na fursa mbalimbali za uwezeshaji.
Nanauka alisema, Serikali imeendelea kuimarisha uratibu wa masuala ya vijana kupitia Wizara hiyo ili kuhakikisha programu zinazotekelezwa na wizara, taasisi za umma na wadau mbalimbali zinaendana na mahitaji halisi ya kundi hilo.
Alisema, mafanikio ya mwaka mmoja yanaonesha umuhimu wa kuwa na mfumo maalumu wa kusimamia ajenda ya maendeleo ya vijana, ikiwemo kuwaunganisha na fursa za kiuchumi, kuwajengea uwezo na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa.
Hafla hiyo ilifanyika chini ya kaulimbiu “Mwaka Mmoja, Vijana Pamoja”, ikiwa na lengo la kuonesha hatua zilizofikiwa, mafanikio yaliyopatikana na mwelekeo wa Serikali katika kuendeleza vijana.
Vile vile, imehusisha maonesho ya bidhaa, huduma na bunifu mbalimbali zinazofanywa na vijana, pamoja na ushiriki wa taasisi za Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo.