Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt. Ashura Katunzi.
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa vyeti na leseni za ubora 3,940 vimetolewa kwa wazalishaji, miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,683.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt. Ashura Katunzi, wakati akielezea mafanikio ya Shirika hilo kuelekea utekelezaji wa dira 2050 kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Alisema, Serikali kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya Shilingi Milioni 300 kila mwaka kwa madhumuni ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote.
“Leseni hizi zimesaidia wazalishaji kuweza kuzalisha bidhaa bora, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao kuweza kuaminika sokoni na pia kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa,” alisema.
Aidha, alisema, Shirika limeendelea na huduma za usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na maeneo ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula na vipodozi kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wa maeneo hayo ili kuendelea kulinda afya za walaji ambapo jumla ya bidhaa 9,731 zilisajiliwa na maeneo 80,836 yalisajiliwa.
Pia, katika kuimarisha ukaguzi wa bidhaa mbalimbali zinazoingia nchini kutoka nchi za nje, TBS huhakiki ubora wa bidhaa na magari yaliyotumika kabla ya kusafirishwa kuja nchini ambapo katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita jumla ya shehena za bidhaa 183,186 zilikaguliwa kabla ya kuingia nchini kupitia mfumo wa Pre-Shipment to Conformity (PVoC) na shehena za bidhaa 426,842 zilikaguliwa baada ya kufika nchini kupitia mfumo wa Destination Inspection (DI).
Mkurugenzi huyo alisema jumla ya magari 249,386 yalikaguliwa “Bidhaa hizi zinakaguliwa kwa lengo la kuiepusha Tanzania kuwa jalala la bidhaa duni pamoja na kulinda afya, usalama na mazingira ya watumiaji.”
Kwa upande wa mafunzo, TBS imeweza kutoa mafunzo kwa jumla ya wadau 6824 wakiwemo wazalishaji wa bidhaa za viwandani na wasindikaji. “Mafunzo hayo yalihusu dhana nzima ya viwango na ubora ambayo yatawawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango na yamewawezesha kupata uelewa mpana kwenye masuala ya udhibiti ubora, hivyo kuwaandaa kuhimili ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.”
Vilevile, alisema TBS imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili kukuza uelewa juu ya masuala ya viwango na udhibiti ubora. Njia hizo ni pamoja na kuanzisha kliniki ya Viwango ambayo inaendelea katika maeneo mbalimbali; pamoja na kushiriki katika makongamano, maonesho, warsha na semina.
Pia, kwa kuandaa mikutano na wadau wa masuala ya viwango, kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya ubora na usalama; na kuendesha kampeni za elimu kwa umma katika ngazi za wilaya.