Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KAMATI ya Pamoja ya kupitia hadidu rejea na utekelezaji wa Tamko la Pamoja baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo, imetakiwa kuweka mbele maslahi ya Taifa, wananchi na Zanzibar.
Akizungumza na wanahabari Septemba 15, 2026, Katibu wa Kamati Maalum, NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Komredi Khamis Mbeto Khamis aliwataka wanakamati hao wasiingize utashi mwingine katika majadiliano hayo.
Komredi Mbeto alisema, Kamati hiyo ambayo ilitangazwa rasmi Septemba 14, 2026 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ijadili bila woga na jambo ambalo lina faida kwa Taifa, ilipe kipaumbele.
“Kama jambo halina faida waachane nalo, hawafungwi na jambo lolote waende kujadili hizo ajenda na kutoa maoni yao,” alisema na kuwabainishia kuwa, wameaminiwa na vyama vyao hivyo wana wajibu.
Komredi Mbeto, alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kutekeleza takwa la Tamko la Maridhiano la kuunda kamati hiyo ya pamoja, amewataka wanakamati wanaoiwakilisha CCM kuzingatia maslahi ya Taifa na chama chao.
”Na mimi niwaambie kwa upande wa wanaCCM, wafahamu kwamba waweke mbele maslahi ya nchi yetu na chama chetu ambacho ndicho kinaaminika na watanzania hadi hivi sasa,” alisema Komredi Mbeto.
Kamati hiyo inayoundwa na watu 10 inatokana na viongozi wakuu wa vyama hivyo Julai 7, 2026 kusaini tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa na imechukua takribani miezi tisa kupata ajenda hizo ambazo sasa zinaenda kujadiliwa na kamati hiyo kisha kutoa maoni yao ambayo yatarudishwa kwenye vyama hivyo kwa hatua zaidi, ikiwa ni safari ya kuelekea kwenye maridhiano ya muafaka wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Zanzibar.