Na Hassan Kimweri, WAF
SERIKALI imewataka wananchi hususan vijana, kupunguza matumizi ya pombe na kuacha matumizi ya dawa za kulevya ili kuepuka changamoto za afya ya akili pamoja na madhara mengine kwa familia na jamii.
Wito huo umetolewa leo Septemba 02, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe wakati akifungua mafunzo kwa wataalamu wa afya ya akili yanayofanyika Mkoani Dodoma huku Serikali ikiendelea kuimarisha huduma za afya ya akili nchini, umuhimu wa kuwekeza zaidi katika kinga na elimu kwa jamii.
“Matumizi ya pombe yaliyokithiri ni miongoni mwa changamoto zinazopaswa kupewa kipaumbele, hasa kutokana na vijana kuanza kutumia pombe katika umri mdogo ambapo hali hiyo inaweza kuathiri masomo, kazi, mahusiano ya kifamilia na uwezo wa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za jamii,” amesema Dkt. Magembe.
Aidha, Dkt. Magembe amesema matumizi yaliyokithiri ya pombe na dawa za kulevya yanachangia vitendo vya ukatili na migogoro katika jamii, huku akisisitiza kuwa mtu anapofikia hatua ya utegemezi mkubwa wa vilevi, kumsaidia kuacha si jambo rahisi na kunahitaji wataalamu, matibabu, muda pamoja na ushirikiano wa familia na jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma Tiba Wizara ya Afya Dkt. Hamadi Nyembea amesema mafunzo hayo yatasaidia jamii kwakuwa yanakwenda kutolewa katika mikoa mbalimbali, hususan katika maeneo yenye mahitaji na matumizi makubwa ya pombe.
“Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuimarisha huduma za afya katika jamii, ikiwemo afya ya uzazi, afya ya mtoto, uzazi wa mpango, magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na afya ya akili,” amesema Dkt. Nyembea.
Mwisho, Dkt. Nyembea amesema jukumu la wataalamu wa afya ni kuwatambua wenye changamoto mapema, kutoa huduma za awali na kuwapeleka katika vituo vya ngazi za juu pale wanapohitaji huduma za kibingwa zaidi, hatua itakayosaidia wananchi kupata huduma kwa wakati na karibu na maeneo wanayoishi.
Serikali imesisitiza kuwa watu wenye changamoto za afya ya akili hawapaswi kunyanyapaliwa wala kutengwa, bali wanapaswa kueleweka, kusaidiwa na kupewa nafasi ya kurejea katika maisha ya kawaida, matibabu ya afya ya akili si dawa pekee, bali yanapaswa kuhusisha familia, jamii na mazingira ambayo mgonjwa anaishi.