Dodoma
RAIS wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, Wakili Boniventure Mwambaja, amesema anaiona Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuwa ni miongoni mwa taasisi bora za maendeleo ya miundombinu barani Afrika kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017.
Wakili Mwambaja ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la TARURA katika Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika uwanja wa Dkt. John Malecela mkoani Dodoma.
Akizungumza baada ya kupata maelezo kuhusu shughuli na mafanikio ya wakala huo, amesema TARURA imeonyesha maendeleo makubwa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara za vijijini na mijini hatua ambayo imechangia kuboresha huduma za usafiri na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Ni dhahiri kuwa TARURA imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya ujenzi na matengenezo ya barabara tangu kuanzishwa kwake. Vilevile, imefanikiwa kuwajengea uwezo watumishi wake wanaosimamia miradi mbalimbali jambo linalodhihirishwa na mrejesho chanya kutoka kwa wananchi”, amesema Wakili Mwambaja.
Ameongeza kuwa ongezeko la mtandao wa barabara zinazopitika katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na utatuzi wa haraka wa changamoto katika maeneo korofi ni ushahidi wa dhamira na ufanisi wa wakala huo katika kuwahudumia wananchi.
TARURA inaendelea kushiriki Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yenye kauli mbiu “Tambua Soko; Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050” kwa kutoa elimu kuhusu majukumu yake, mafanikio yaliyofikiwa na huduma mbalimbali zinazolenga kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini na mijini nchini.