Na Aisha Swahibu, WAF
TANZANIA imeendelea kupiga hatua kubwa katika mwitikio wa VVU, huku matokeo ya Utafiti wa Athari za VVU Tanzania (THIS 2022/2023) yakionyesha kuwa asilimia 82.7 ya watu wazima wanaoishi na VVU wanajua hali zao za maambukizi, asilimia 97.9 ya waliogundulika wanatumia dawa za kufubaza virusi (ART), na asilimia 94.3 ya waliopo kwenye matibabu wamefikia ukandamizaji wa virusi.
Mafanikio hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, Julai 8, 2026, wakati wa kikao kazi na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na VVU na UKIMWI (UNAIDS), Winnie Byanyima, kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.
Dkt. Samizi amesema matokeo hayo yanaonesha kuwa Tanzania ipo kwenye mwelekeo sahihi wa kufikia malengo ya kimataifa ya 95-95-95 na kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.
Amepongeza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Tanzania na UNAIDS, akisema umechangia kuimarisha mwitikio wa taifa dhidi ya maambukizi ya VVU, kuandaliwa kwa ramani ya uendelevu wa mwitikio wa VVU nchini pamoja na kuboresha maandalizi ya ombi la ushirikiano wa Mzunguko wa Nane wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund Grant Cycle 8).
“Matokeo haya yanaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha watu wanaogundulika na maambukizi ya VVU wanaanza matibabu kwa wakati na kuyafuata ipasavyo. Kazi iliyopo sasa ni kuwafikia wale ambao bado hawajui hali zao za maambukizi, hususan vijana, wasichana balehe na wanawake vijana,” amesema Dkt. Samizi.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za upimaji wa VVU kupitia kampeni za kijamii, huduma za kujipima, vituo vya upimaji vinavyohama, huduma katika maeneo ya kazi pamoja na ujumuishaji wa huduma za VVU na Kifua Kikuu, afya ya mama na mtoto na huduma nyingine za msingi.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kupanua huduma za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU kupitia matumizi ya dawa kinga (PrEP), utoaji wa dawa za ART katika jamii, utoaji wa dawa za matumizi ya miezi mingi pamoja na kuongeza ushiriki wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu na maeneo wanayoishi.
“Kwa kuendelea kushirikiana, tutaweza kulinda mafanikio tuliyoyapata na kutimiza azma ya kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030,” amesisitiza Dkt. Samizi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kudhibiti maambukizi ya VVU na kuboresha upatikanaji wa huduma za kinga, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa.
Byanyima amesema UNAIDS itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mifumo ya afya, kuhakikisha mwitikio wa VVU unakuwa endelevu na kusaidia juhudi za kufikia malengo ya Kimataifa ya kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.