WAZIRI Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuna haja ya kutafuta mbinu mpya ya kukieneza Kiswahili baada ya kuwa kimepata hadhi ya kimataifa.
“Kadiri Kiswahili kinavyoendelea kupata hadhi ya kimataifa, ni muhimu sasa kuanza kutazama hatua inayofuata ya kukieneza duniani. Mataifa mengi yamefanikiwa kueneza lugha na utamaduni wao kupitia vituo vya utamaduni vilivyoanzishwa katika nchi mbalimbali duniani,” amesema.
Ametoa wito huo wakati akizungumza na washiriki waliohudhuria kilele cha Maadhimisho ya Tano ya Siku ya Kiswahili Duniani kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za makao makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa.
“Serikali itaendelea kuimarisha matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kupitia elimu, tafiti, uchapishaji, tafsiri, teknolojia za kidijiti na diplomasia ya lugha. Tutaendelea kushirikiana na UNESCO, nchi mbalimbali, vyuo vikuu, taasisi za kimataifa na wadau mbalimbali katika kuendeleza lugha hii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema sasa hivi Kiswahili kimeshatambulika kuwa lugha rasmi ya EAC na SADC. “Kiswahili ndiyo utambulisho wetu wana jumuiya ya Afrika Mashariki. Mtu akiongea Kiswahili anajulikana kuwa anatokea Tanzania, Burundi, Congo au Sudan Kusini. Na pia kimekuwa moja ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika (AU),” amesema.
Amesema kwa mujibu wa wataalamu wa lugha, Kiswahili kinazungumzwa na watu kati ya milioni 300 hadi milioni 500 na idadi hiyo inaendelea kuongezeka kutokana na matumizi yake katika elimu, biashara, vyombo vya habari, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Prof. Khaled El-Enany aliwaeleza washiriki wa maadhimisho hayo kwamba shirika lake limesaidia kufadhili uandaaji wa kamusi ya Kifaransa kwenda Kiswahili.
“Mbali na matumizi ya kawaida kwa watalii au watu wanaojifunza lugha, tunatarajia kwamba uwepo wa kamusi hiyo na nyaraka nyingine kutasaidia kuongeza fursa kwa walimu na wanafunzi wanaojifunza Kifaransa na Kiswahili,” amesema.