RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali zote mbili za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) zitaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za kiuchumi zinazosababishwa na mgogoro wa vita vya Mashariki ya Kati, hususan kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta.
Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo leo, tarehe 27 Mei 2026, alipohutubia Baraza la Eid lililofanyika katika Uwanja wa Kufurahishia Watoto Tibirinzi, Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema hali inayoendelea Mashariki ya Kati inaleta changamoto kubwa za kiuchumi duniani na kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi, hivyo Serikali itaendelea kuchukua hatua mahsusi za kupunguza athari hizo kwa wananchi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewaomba wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali katika juhudi zake za kukabiliana na hali hiyo pamoja na kuhimiza kuombewa amani na maridhiano duniani kwa ajili ya ustawi wa watu wote.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi amepongeza Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kupitia Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana pamoja na Umoja wa Taasisi Zinazosafirisha Mahujaji Zanzibar (UTAHIZA) kwa ushirikiano wao mzuri katika kufanikisha huduma za usafirishaji wa mahujaji wa Zanzibar.
Amesema ibada ya Hijja inafundisha umuhimu wa umoja, mshikamano na usawa wa wanadamu wote mbele ya Mwenyezi Mungu bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazowasilishwa na taasisi zinazoshughulikia safari za Hijja ili kuweka mazingira bora yatakayowezesha waumini wengi zaidi kutimiza Nguzo ya Tano ya Uislamu.
Vilevile, ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia pamoja na maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa katika kuhakikisha mahujaji wa Tanzania wanapata huduma na mazingira mazuri wakati wa utekelezaji wa ibada ya Hijja.
Mapema baada ya kuwasili katika Baraza hilo, Rais Dkt. Mwinyi alipokea salamu na kukagua gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Polisi Tanzania.