Meneja wa Kitengo cha Bandari, Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Alfred Shungu akikagua mtungi maalum unaotumika kuhakiki ujazo wa gesi asilia katika vituo vinavyotumika kujaza gesi hiyo kwenye magari. WMA hufanya kazi ya kuhakiki Pampu zinazotumika kujazia gesi ili kumlinda mlaji/mnunuzi na muuzaji, wote wapate faida stahiki.
Na Mwandishi Wetu
KATIKA kuelekea siku ya vipimo duniani inayotarajia kufanyika Mei 20, 2026, imeelezwa vipimo sahihi ni msingi wa sera zenye matokeo, biashara yenye haki na maendeleo endelevu.
Kauli hiyo imetolewa na Mchumi Mwandamizi wa Wakala wa Vipimo (WMA) Fadhil Msane, wakati akichambua jinsi sera za Kitaifa zinavyochangamana na matumizi sahihi ya vipimo katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.
Msane alisema, data na takwimu za vipimo ni muhimu kwa watunga sera, ambapo alitolea mfano Serikali inapopanga bei ya mafuta kwa lita, WMA jukumu lao ni kuhakikisha kama kweli lita moja imetimia.
“Mteja akitoa Shilingi 3,000 apate kipimo sahihi, iwe lita moja yake, asipunjwe, kwahiyo kwa kulitambua hilo utaona vipimo ni nguzo muhimu ambayo haiwezi kukosekana,” alisema Msane.
Aidha, alisema katika kutekeleza majukumu yao, wakiwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, wanaongozwa na sera tatu; sera ya biashara, sera ya maendeleo endelevu ya viwanda na sera ya wajasiliamali wadogo na wa kati.
“Ukiangalia sera hizi zinatutaka kuhakikisha wazalishaji wa ndani wanazingatia vipimo sahihi viweze kufikia masoko ya Kikanda na Kimataifa, lakini kulinda viwanda vyetu na kuhakikisha vinazalisha kwa vipimo sahihi ili nao wafike kwenye masoko ya Kikanda na Kimataifa,”
“Pia, bidhaa zinazofungashwa zinazoingia nchini, ziwe kwenye vipimo sahihi ili kuvilinda viwanda vyetu vya ndani, kwahiyo ukiangalia mnyororo mzima kuanzia shambani hadi kwenda dukani, na kutoka kiwandani hadi bandarini, lazima tuhakikishe tunazingatia vipimo sahihi,” alisema Msane.
Msane alisema, dira ya Taifa ya 2050, inaelekeza nchi kufikia uchumi wa Kati wa Juu, hivyo WMA kama nguzo muhimu, data na takwimu zitawasaidia watunga sera katika kufanya maamuzi ya kufikia malengo hayo.
“Sera bora zitahitaji takwimu sahihi na takwimu sahihi utazipata kwa vipimo sahihi, vipimo sahihi vitapatikana kwa mfumo Madhubuti ambao tunausimamia sisi Wakala wa Vipimo,” alisema, Msane na kuitaka jamii kuendelea kutumia vipimo sahihi.