Na Josephina Lupasha, MAELEZO
SERIKALI imesema itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafiri wa reli, anga, maji na barabara katika Jiji la Mwanza kufuatia Jiji hilo kuchangia Shilingi Trilioni 14.8 ambazo ni sawa na asilimia 7.2 katika Pato la Taifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema hayo, Machi 22, 2026 Jijini Mwanza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya Serikali katika maeneo mbalimbali.
Amesema mchango huo unaonesha wazi nafasi muhimu ya mkoa katika kuendesha gurudumu la uchumi wa nchi akiwapongeza wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa kuchangamkia fursa za maendeleo, juhudi na kazi ambazo zimekuwa chachu ya mafanikio hayo makubwa.
“Mkoa huu unachangia takriban Shilingi Trilioni 14.8 katika pato la Taifa na ukiwa ni mkoa wa pili kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la Taifa, unachangia kwa asilimia 7.2” amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa hali hiyo imeufanya mkoa wa Mwanza kuwa kitovu cha fursa za kiuchumi kwa nchi jirani za Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Sudan Kusini.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa kutenga na kuidhinisha bajeti kwa mkoa huo ambapo jumla ya shilingi bilioni 629.4 zimetolewa ili kutekeleza shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo.
Ameongeza kuwa Serikali imetekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa meli ya MV Mwanza na kukamilisha daraja la JP Magufuri (Kigongo–Busisi), ambayo imefungua ukurasa mpya wa usafiri na biashara kama nyenzo ya kiuchumi katika Mikoa ya Kanda ya ziwa.
Pia, amesema mafanikio hayo yameongeza fursa za ajira, kurahisisha usafirishaji wa watu, bidhaa, kuchochea uwekezaji zaidi na kuufanya mkoa wa Mwanza kuendelea kuwa kitovu muhimu cha uchumi nchini.