Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa ruzuku ya kiasi cha Shilingi Bilioni 5.4 kwenye mradi kuzalisha umeme wa maji Lupali, wenye uwezo wa kutoa Kilowati 317.
Ruzuku hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kusaidia wawekezaji wanaozalisha umeme hususan maeneo ya Vijijini.

Akizungumza katika ziara ya Jukwaa la Wahariri walipotembelea mradi wa Lupali ulioko Njombe Meneja wa Usaidizi wa kiufundi kwa Wawekezaji kutoka REA Mhandisi Emmanuel Yesaya amesema REA imetoa ruzuku kwa awamu tano zenye jumla ya Shilingi Bilioni 5.4.
Amesema hizo zimesaidia ujenzi wa kituo cha uzalishaji wa umeme sambamba na miundombinu ya usambazaji katika kituo cha Imiliwaha Sisters Convent pamoja na vijiji vya Boimanda, Kitulila na Matola.
Mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Watawa la Benedictine Sisters of Getrud Convent Imiliwaha umefikia asilimia 99 na kazi zilizokamilika hadi sasa ni ujenzi wa kizuizi cha maji na mtaro wa kupitisha maji ya mafuriko.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri TEF Deodatus Balile ameipongeza REA kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha takriban shilingi bilioni 5.4 za kuendeleza na kutekeleza mradi huo unaokwenda kuongeza ubora wa upatikanaji wa umeme kwenye mkoa wa Njombe.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi Sista Imakulata Mlowe, amesema kuwa mara baada ya mradi kukamilika, umeme utakaozalishwa utauzwa moja kwa moja kwa TANESCO ambapo tayari mkataba wa kuuziana umeme umeshasainiwa.
Ameongeza faida za mradi utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi kwa matumizi ya nyumbani na biashara na kupinguza matumizi ya nishati isiyo rafiki na mazingira.
Ziara hiyo ya TEF mkoani Njombe imelenga kupitia utekelezaji wa miradi ya REA inayotekelezwa katika huo sambamba na kupitia maendeleo ya waendelezaji wadogo wa miradi ya kuzalisha umeme hapa nchini na kupatiwa ufumbuzi.