Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 2, 2026, alipokuwa akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislamu wa Msikiti wa Ijumaa wa Unguja Ukuu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kuungana nao katika ibada ya Sala ya Ijumaa.
Amesema ujenzi wa Daraja la Uzi Ng’ambwa pamoja na barabara zake, ambao kwa muda mrefu umekuwa kilio cha wananchi, umefikia hatua nzuri na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi minne ijayo.
Rais Dkt. Mwinyi ameielezea hatua hiyo kuwa ni mafanikio makubwa kwa wananchi wa eneo hilo na Zanzibar kwa ujumla.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kujipanga kutafuta ufumbuzi wa changamoto nyingine zinazowakabili wananchi, ikiwemo miundombinu ya barabara na upatikanaji wa maji safi na salama.
Katika hatua hiyo, ameeleza kuwa Serikali itawatuma wataalamu wake katika siku za karibuni ili kufanya tathmini na kubaini njia bora za kutoa ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hizo.
Rais Dkt. Mwinyi amewanasihi wananchi kuendelea kudumisha amani na kuiombea nchi, akisisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo.
Amesema kuwa kuwepo kwa amani kunawezesha Serikali kukusanya mapato kwa ufanisi na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kiwango kikubwa zaidi.
Kwa muda mrefu sasa, Rais Dkt. Mwinyi ameendelea kuimarisha utaratibu wa kuungana na waumini wa Dini ya Kiislamu katika ibada ya Sala ya Ijumaa kwenye misikiti mbalimbali, mijini na vijijini.