Na Mwandishi Wetu
UKIFUATILIA kinachoendelea mitandaoni kwasasa hasa ukiwa mbali na Tanzania, unaweza kuamini kile kinachoelezwa kwamba, chama cha Mapinduzi (CCM) kimechokwa na kina hali mbaya kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kwamba, CCM hakiwezi kurudi tena madarakani, lakini kama ulipata bahati ya kuhudhuria mikutano ya kampeni ya chama hicho hususani ile ya mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan, picha uyayoipata ni tofauti kabisa.
Nilikuwepo kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika Agosti 28, 2025 kwenye viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam, niliona makundi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam walivyomiminika kwenye viwanja hivyo kutoka maeneo mbalimbali.
Nikabahatika kuhudhuria mikutano mingine ya mikoa takribani mitatu, hali ni ileile; mikutano ilikuwa na watu wengi ambao walikwenda kusikiliza nini chama hicho kimefanya kwa miaka mitano iliyopita na nini watafanya iwapo watapewa ridhaa ya kuongoza kwa miaka mitano ijayo.
Mbali na mikutano hiyo, mkutano wa mwingine ambao ulifanyika Kinyerezi Oktoba 22, nao ulikuwa funga kazi, hadi kufika majira ya Saa tano asubuhi, uwanja ulikuwa umejaa, hakukuwa na pakuweka mguu, huku wananchi kwa makundi walionekana wakiendelea kumiminika.
Niliona Kundi kubwa la vijana ambao wanaitwa ‘Gen Z,’ wanaochochewa kuandamana, wakiimba nyimbo za kumsifia Rais Samia na Chama cha Mapinduzi, hali ilivyokuwa katika uwanja wa TANESCO, Buza Jijini Dar es Salaam Oktoba, 23, 2025 ulinipa picha kubwa zaidi ya kukubalika kwa Dkt. Samia na chama hicho tawala.
Kuanzia hapo nikabaini kwamba, mengi yanayozungumzwa mitandaoni, ni porojo za watu kujifurahisha, lakini ukweli wa mambo upo mitaani. Huko ndio utasikia hisia za kweli za Watanzania ambao bado wana matumaini makubwa na CCM na wanamkubali Rais Samia.
Ni wananchi ambao wanaona kwa macho yao yaliyofanyika, ni vigumu kuwaaminisha kwamba hakuna chochote ambacho Rais Samia amekifanya kwa miaka minne aliyokaa madarakani.
Ni mashuhuda wa miradi mikubwa ya kimkakati aliyoikamilisha baada ya kupokea nchi, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli.
Wengi walipata hofu, wakaamini kwamba miradi hiyo haiwezi kukamilika, lakini Rais Samia kama alivyoahidi wakati anaingia madarakani akitumia kauli ya ‘kazi inaendelea,’ amekamilisha miradi hiyo na kuongeza mingine.
Kazi kubwa iliyofanyika, ndio ambayo inampa uhakika wa kupata ushindi wa kishindo na kurejea tena madarakani kwa ajili ya kutekeleza Ilani mpya ya CCM iliyozinduliwa Mei 30, 2025, itakayotekelezwa kwa Miaka Mitano ijayo 2025-2030.
Ilani hiyo imesheheni mambo makubwa yanayotoa picha kubwa ya Tanzania ambayo Rais Samia anatamani kuiona, ambayo inaenda sambamba na dira ya maendeleo 2050, ambayo nayo ukiisoma utagundua, Tanzania ijayo ambayo misingi yake inajengwa na Serikali ya Awamu ya Sita, itakuwa ya mfano Barani Afrika.
Kwa maana hiyo, mati unaojitokeza kwenye mikutano ya kampeni za CCM inatupa ujumbe tosha kwamba, watanzania wanajua ukweli, wamekataa kulishwa propaganda, ndio maana kupitia utafiti uliotolewa hivi karibuni na Kituo cha Sera za Kimataifa-Afrika – Centre for International Policy-Africa (CIP-Africa) asilimia 83 ya Watanzania wamesema watashiriki uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Matokeo ya utafiti huo yametolewa na Mkurugenzi wa Utafiti na uchapishaji wa Kituo hicho, Thabiti Mlangi ambapo alisema, wamefanikiwa kuwahoji wananchi 1,976, wote wakiwa na sifa za kushiriki uchaguzi huo kwa kujiandikisha na kuwa na Vitambulisho vya Mpiga kura.
Aidha, ameeleza kuwa asilimia 53 ya wananchi hao wamekiri kushiriki kwenye Mikutano ya Kampeni za Vyama vya siasa, asilimia 76 kati yao wakihudhuria Mikutano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), asilimia 15 wakihudhuria Mikutano ya ACT – Wazalendo, asilimia 7 wakihudhuria Mikutano ya Vyama vya siasa zaidi ya Kimoja na asilimia 2 wakihudhuria Mikutano ya Chama cha CHAUMMA.
“Kuhusu ushiriki katika mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Uraisi, ubunge na udiwani, asilimia 53 ya walioshiriki utafiti wameshiriki katika mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa. Kati ya waliohudhuria kwenye mikutano ya kampeni, asilimia 76 walihudhuria mikutano ya kampeni ya CCM, asilimia 2 walishiriki mikutano ya kampeni ya CHAUMMA, asilimia 15 wameshiriki mikutano ya kampeni ya ACT-Wazalendo. Aidha, asilimia 7 wameshiriki katika mikutano ya kampeni ya chama zaidi ya kimoja,” amekaririwa Mlangi.
Kwa maana hiyo, hakuna shaka yoyote kwamba Jumatano, Oktoba 29, maandamano yatakayooneekana mitaani ni ya kwenda kupiga kura, sio yale yanayohamasishwa ya kutaka kuvuruga uchaguzi na hiyo ni dalili njema kwa Rais Samia ambaye hakuna shaka yoyote kwamba, atashinda kwa kishindo; takwimu na hali halisi inathibitisha hilo.