Na Mwandishi Wetu, Pemba
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amesema, wananchi wa Pemba wanastahili kumchagua tena mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Hussein Mwinyi kutokana na mambo makubwa aliyowafanyia.
Mbeto alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa kuhitimisha kampeni kwa upande wa Pemba uliofanyika Oktoba 23, kwenye uwanja wa michezo wa Micheweni, Mkoa wa Kaskazini, ambapo alitaja mambo kadhaa ambayo yamefanyika kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Awamu ya nane.
Miongoni mwa mambo hayo ni uboreshaji wa miundombinu ya Barabara, ambapo alisema zimejengwa Barabara 83 visiwani humu, ikiwemo ya kutoka Chake Mkoani, Chake Wete, “Wete umetupelekea Barabara 21, Micheweni umetujengea barabara 16, Chake Barabara 22,”
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya elimu Mbeto alisema, Rais Dkt. Mwinyi amewajengea maghorofa 13, “Kusini tuna maghorofa nane, Kaskazini maghorofa Matano, skuli za msingi za kawaida 20, umeendelea kutufanyia ukarabati na kutujengea mpya, zimejengwa shule za sekondari 11, kuna shule za maandalizi 21, haya mmepata kuyaona?”
Kwa upande wa maji, Mbeto alisema Rais Dkt. Mwinyi amewajengea matanki Matano kwa awamu ya kwanza ya uongozi wake, awamu ya pili iwapo watamchagua, kuna mradi mwingine wa matanki ya maji utatekelezwa.
“Mheshimiwa Rais umetujengea hospitali kila wilaya, umeboresha maisha yetu kwenye pensheni jamii na pensheni ya kawaida, hapa Micheweni unatujengea viwanja vya michezo, kwa kweli Mheshimiwa rais wananchi wa Pemba wana haki ya kukuchagua na watakuchagua,” alisisitiza Mbeto.
Mbali na hayo, Mbeto alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kudumisha amani na utulivu kwa kipindi chote cha kampeni, ambapo tangu zilipoanza hadi sasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, hakuna mwananchi yeyote aliyepata msukosuko.
“Hakuna aliyepigwa, hakuna aliyesukumwa, umewaunganisha ndugu, ni jambo kubwa, sio wale wanaopita na kubagua watu na kuwatenga. Mtu anasimama anasema eti Rais Mwinyi mpita njia, kwamba yeye hawezi kushindwa na mpita njia, Dkt. Mwinyi ni mpita njia?” alihoji Mbeto.