KATIKA kipindi cha miaka minne, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendelea kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora za mawasiliano, hususan wale wanaoishi vijijini na maeneo ya pembezoni.
Kupitia ushirikiano na watoa huduma za mawasiliano ya simu, UCSAF imefanikisha kufikisha huduma za mawasiliano katika vijiji 1,142 nchini. Utekelezaji huo umehusisha ujenzi wa minara 1,225 ya mawasiliano ambayo imewezesha wananchi wapatao Milioni 16.8 kunufaika na huduma hizo muhimu.
Utekelezaji huu umegharimu ruzuku inayokadiriwa kufikia Shilingi Bilioni 187.8, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kupanua wigo wa mawasiliano na kuondoa pengo la kidijitali kati ya mijini na vijijini.