Mbeto: Tutamlinda Rais Samia kwa gharama yoyote

0

Na Mwandishi Wetu, Pemba

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kitawalinda kwa gharama yoyote Marais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Huseein Ali Mwinyi dhidi ya
Vibaraka na Mamluki wachache wanaotishia Amani na Umoja wa Kitaifa nchini.

Pia, CCM kimesema hila na njama za wakorofi wowote hazitafua dafu kwani Watanzania muda wote wako madhubuti.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar , Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis ameitaja thamani ya uhuru na Umoja wa Kitaifa ulioasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na mwenzake Sheikh Abeid Amani Karume vitalindwa kwa nguvu zote.

Mbeto alisema, Serikali za CCM hazitingishwi aidha na makundi ya Wanasiasa au Wanaharakati vinyangarika wasiojitambua kwa tamaa ya kupata fedha.

“Watanzania Hawajalala, bado wako macho na makini muda wote, Hawatawatupa mkono Marais Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi dhidi ya vitishio vya wanasiasa malaya waliokubali kuupiga mnada Utu wao,” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema, Wanasiasa na Wanaharakati wenye nia ya kuiweka rehani Amani ya Taifa letu, watakabiliwa na mwisho wa aibu na fedheha isiokadirika.

“Wasifikiri kwa kununuliwa kwao na vipande vya sarafu nao wangeweza kuwanunua Watanzania. Toka sasa kila mmoja wao ajitafakari na kusalimu amri. Watanzania si malaya au waganga njaa,” alieleza.

Katibu huyo Mwenezi alisema, CCM kwa wakati huu kikiendelea na kampeni zake nchini, kinawataka Watanzania kutobabaishwa na propaganda za bei rahisi katika mitandao ya Kijamii badala yake wachapekazi na kuzalisha mali.

“Ifikapo Oktoba 29 Mwaka huu Wananchi tokeni, nendeni mkapige kura vituoni bila longolongo. Nendeni mkatimize matakwa ya kikatiba, kiraia na kidemokrasia,” alisisitiza.

Vike vile, Mbeto aliwataka watanzania kila mmoja atumie haki yake ya kuchagua bila kupoteza kura na kuwachagua wagombea wa CCM, Marais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.

“Uchaguzi utafanyika. Matokeo yatatangazwa, Washindi watajulikana, maisha baada ya uchaguzi yataendelea kama kawaida,” alisema Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here