SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kutekeleza mradi wa usambazaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shule za sekondari za umma nchini.
Kupitia mradi huu, UCSAF imefanikiwa kufikisha vifaa vya TEHAMA katika shule 1,121, ambapo kila shule imenufaika kwa kupatiwa kompyuta 5, projekta 1 na printer 1.
Lengo ni kuhamasisha na kukuza uelewa wa TEHAMA miongoni mwa wanafunzi, ili waweze kutumia teknolojia kwa ufanisi katika kujifunza na kujiandaa na fursa za kidijitali wanapofikia vyuo vikuu au soko la ajira.
Mradi huu pia unawasaidia walimu kwa kuwapatia nyenzo za kisasa za kufundishia, hivyo kuongeza ubora wa elimu na ufanisi wa ufundishaji darasani.
Hadi kufikia Desemba 2024, Serikali kupitia UCSAF ilikuwa imefikisha vifaa hivyo vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 5.94, na utekelezaji wa awamu zinazofuata unaendelea kwa lengo la kuhakikisha shule zote nchini zinapata fursa sawa za TEHAMA.