Dkt. Mwinyi: Vijana kataeni siasa za ubaguzi na chuki

0

WETE, Kaskazini Pemba

MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa wakati umefika kwa vijana kukataa siasa za ubaguzi na chuki ambazo zinahatarisha umoja na mshikamano wa Wazanzibari.

Amesema tangu Serikali ya Awamu ya Nane iingie madarakani, imekuwa ikisimamia kwa dhati umoja, amani na mshikamano, na kuwataka vijana kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa hatima ya Taifa imo mikononi mwa vijana, kwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wananchi ni vijana, hivyo amewasihi kulinda amani na umoja wa nchi kwa nguvu zao zote.

Amesema vijana wamethibitisha uwezo wao mkubwa katika uongozi, jambo aliloliona kupitia utendaji wao katika Serikali ya Awamu ya Nane.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na makundi ya vijana wa CCM Kisiwani Pemba, katika mwendelezo wa mikutano yake ya kampeni, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amebainisha kuwa katika Serikali ijayo baada ya ushindi wa CCM, nafasi nyingi za uteuzi zitatengewa kwa vijana, akisema wale aliowateua katika awamu iliyopita walionesha uwezo, nidhamu na ufanisi mkubwa.

Aidha, Dkt. Mwinyi ameahidi ajira nyingi zaidi kwa vijana kupitia nafasi za Serikali na uwekezaji mpya katika sekta za viwanda, ambazo zitaleta fursa za ajira kwa wingi.

Amesema Serikali imejipanga kuelekeza nguvu zote katika kutatua changamoto za ajira, ikiwemo utoaji wa mikopo isiyo na riba na mafunzo ya stadi za kazi ili vijana waweze kujiajiri na kuajiri wengine.

Ameongeza kuwa CCM ina uhakika wa ushindi kutokana na uimara wa jumuiya zake ikiwemo UVCCM, UWT na Wazazi, ambazo zimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wapiga kura na kulinda misingi ya amani wakati wa uchaguzi.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali ijayo itatoa kipaumbele maalum kwa vijana wa makundi ya hamasa waliyojitolea kushiriki kikamilifu katika kampeni, na ameiagiza UVCCM kuandaa mapema orodha ya vijana hao ili waingizwe katika mipango ya ajira na maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here