Teknolojia, maarifa mapya kutumika kukabiliana na changamoto za uhifadhi

0

KATIBU Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema teknolojia za kisasa na maarifa mapya vitakuwa nguzo mpya ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu maeneo mbalimbali nchini.

Dkt. Abbasi ameyasema hayo Oktoba 6, 2025, alipofika Malwilo, Meatu na kisha Itilima katika mkoa wa Simiyu katika mwendelezo wa oparesheni maalum ya kuongeza vifaa vya kisasa kwa askari wa Uhifadhi ili kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu.

Wakati kwa upande wa Meatu amekabidhi ndege nyuki (drones), na kupata ripoti ya kufungwa jumla ya visukuma mawimbi 7 kufuatilia mienendo ya tembo, pia Wizara imesambaza mabomu baridi katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama, operesheni maalum imeendeshwa Wilayani Itilima kutokana na tatizo mahsusi la fisi.

Akizungumza na maafisa na askari wa Uhifadhi walioshiriki katika oparesheni maalum ya kukabiliana na fisi wilayani Itilima, Dkt. Abbasi amewapongeza kwa ujasiri na kuwaokoa wananchi huku pia akiitaka jamii kushiriki vyema.

“Hapa Itilima ambako kumekuwa kukiibuka changamoto ya fisi wanaoleta kadhia katika maisha ya binadamu na mifugo yao, tumeweka na nimekagua kikosi maalum chenye askari mchanganyiko ambako pia vifaa vya kisasa kama ndege nyuki, pikipiki za doria na mabomu baridi nimevikabidhi rasmi lakini ni vyema tukaendelea kushirikiana na jamii na wazee wa kimila na jadi kukomesha tatizo hili,” alisema.

Aidha, ameeleza kuwa Wizara kwa sasa inapitia upya Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Wanyama Wakali na Waharibifu ili kuja na maarifa mapya zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here