BODI ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) imepongeza ubora wa kazi za ujenzi wa Mradi wa Masasi Commercial Complex, unaotekelezwa na NHC wilayani Masasi, mkoani Mtwara.
Katika ziara yao ya ukaguzi, wajumbe wa Bodi walionesha kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo ambao unajengwa kwa viwango vya juu vya ubora na umahiri wa kisasa.
Jengo hilo la biashara lenye mvuto wa kipekee limepata wapangaji kwa asilimia 100, ikiwa ni ishara ya uhitaji mkubwa wa majengo bora ya kibiashara katika eneo hilo.
Mradi wa Masasi Commercial Complex unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 2025, na ukikamilika utachochea shughuli za biashara, kuongeza ajira na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Masasi kwa ujumla.