VIJIJI tisa mkoani Kigoma sasa vimefikiwa kwa huduma ya maji ya uhakika kwa kukamilishwa kwa mradi wa maji wa Buhingu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Grundfos Foundation Poul Due Jensen kutoka Denmark na ujumbe wake wa watu 11 wametembelea mradi huo.
Mradi huo ni mmoja wa miradi 11 iliyotekelezwa mkoani Kigoma kwa Ufadhili wa Kampuni hiyo ambapo mradi wa Buhingu utahudumia vijiji vya Buhingu, Mgambo, Nkonkwa, Katumbi. Kalilani, Igalula, Ndele, Lagosa na Rukoma.
Kazi zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji katika mto Kabezi unaoanzia katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale, uwekaji wa mfumo wa nishati ya umeme Jua wa 54kW, ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha maji yenye urefu wa kilomita 5.3, matangi mawili yenye ujazo wa lita 150,000 na lita 500,000, mabomba ya kusambaza maji yenye urefu wa kilomita 44 pamoja na vituo vya kuchotea maji vya Jamii 47.
Mradi huu umefanikishwa na RUWASA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto Duniani (UNICEF) kwa ufadhili wa Grundfos Foundation kwa gharama ya shilingi bilioni 2.7 na kunufaisha zaidi ya wananchi elfu 64.