SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) Oktoba 4, 2025 limefanya kikao maalum na wateja wake wanaomiliki nyumba katika Mradi wa Morocco Square, kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Kambarage House, jijini Dar es Salaam.
Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa kuchagua viongozi wa Umoja wa Wamiliki wa Nyumba za Morocco Square, ambao watakuwa kiunganishi kati ya wamiliki hao na Shirika la Nyumba la Taifa katika masuala yanayohusu uendeshaji na utunzaji wa jengo hilo la kifahari.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Miliki wa NHC, France Bahangarwa, alitoa elimu kuhusu mamlaka na majukumu ya viongozi watakaoteuliwa, akisisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo imara wa usimamizi wa pamoja.
“Umoja wa wamiliki wa nyumba za Morocco Square unatakiwa kuwa na fundi msimamizi maalum ambaye atahudumia maeneo ya pamoja kama lifti, ngazi, jenereta na huduma nyingine mtambuka,” alisema France.
Aidha, alieleza kwa kina kuhusu michango ya kila mwezi itakayohitajika kuendesha huduma hizo za pamoja, akifafanua aina ya gharama zinazopaswa kugawanywa na wamiliki wote kwa uwiano unaofaa.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa NHC, Scolastica Kilagane, alibainisha kuwa Shirika limejipanga kuhakikisha wateja wote wa Morocco Square wanapatiwa hati miliki zao, jambo litakalowatambulisha rasmi kama wamiliki halali wa nyumba wanazomiliki.
“Tunataka kila mmiliki awe na nyaraka kamili za umiliki wake. Hii itaimarisha uwazi na uhalali wa umiliki wa nyumba katika Morocco Square,” alisema Kilagane.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa uchaguzi wa viongozi wa Umoja wa Wamiliki wa Nyumba za Morocco Square, hatua iliyopokelewa kwa furaha na washiriki kama ishara ya mwanzo mpya wa ushirikiano, uwajibikaji na utulivu katika jengo hilo la kisasa.