Mbeto: SMZ hata ikijenga barabara za dhahabu, ACT watapinga

0

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema upinzani wa Zanzibar unachojua ni kupinga maendeleo kwasababu tu yemeletwa na SMZ, hivyo hata kama zitajengwa barabara za dhahabu upinzani utapinga.

Pia, CCM kimekumbusha hata Nabii Yusuf alipingwa na makuhani wa Misri, aliposhika madaraka akiwa Mtendaji Mkuu wa dola ya kifalme huko Misri.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC ya CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis aliyesema mantiki ya kuwepo upinzani si kupinga na kubeza hata kwa mambo ya msingi.

Mbeto alisema, anashangaa kuuona upinzani hususan ACT Wazalendo, bila aibu viongozi wake wamekuwa wakipinga juhudi za maendeleo ya kisekta yanayoonekana.

Alisema, SMZ chini ya CCM, hata ikijenga Barabara za dhababu, Majengo ya shule kwa kutumia matofali ya Almasi na lulu, ACT kitabeza na kuita huo ni mkaa wa kuni za mikarafuu.

Mbeto alikitaja kitendo cha upinzani kupinga maendeleo, haukuanzishwa na ACT, kwani wapinzani wa ASP chini ya Hayati Rais Mzee Abeid Amani Karume pia walimpinga alipoleta maendeleo.

“Maendeleo hayakuwepo Zanzibar enzi za ukoloni. Bila aibu vibaraka na wapinga maendeleo dhidi ya serikali ya ASP hawakuacha kubeza. Wapinzani wa ASP walidai SMZ haijafanya lolote,” alisema Mbeto.

Pia, Katibu huyo Mwenezi alisema, hata Nabii Yusuf alipingwa na wapinzani wake asifanikishe sekta ya Kilimo cha umwagiliaji na kujenga maghala, hivyo ACT kinapopinga maendeleo ni asili ile ile ya upinzani.

“Makuhani wa Misri walimbagua Nabii Yusuf wakidai hana asili ya Misri. Wakamwita mshamba toka kijijini Canaan huko Palestina. Akafanyiwa vituko akwame kuleta maendeleo. Alisimama imara akabadili Misri kwa muda mfupi,” alieleza.

Katibu Mwenezi huyo alisema, kwa bahati nzuri wananchi wa Zanzibar wameshapevuka kifikra na kupata mwamko, hivyo wanajua kutofautisha ukweli na porojo za wanasiasa uchwara.

“Wananchi wameshuhudia shule za ghorofa zikijengwa, barabara, masoko, Viwanja vya Ndege, Bandari na Madaraja yakijengwa. Wanajua kutofautisha kati ya Maendeleo na Wa,naSiasa wapiga maneno majukwani,” alieleza.

Mbeto alisema, hata Mzee Karume alipotekeleza malengo ya ASP na ya kimajumui hatimae Tanganyika na Zanzibar zikaungana, alichekwa na wapinzani wake.

Katibu huyo Mwenezi alisema, tabia ya kupinga kila kitu imekuwa mila, desturi na utamaduni kwa upinzani wa Zanzibar, lakini kwa Maendeleo yaliofanyika, kila mwananchi sasa amejua ukweli.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here