TUENZI AMANI YETU: Tanzania ni nchi salama zaidi Afrika Mashariki

0

Na Chief Mussa Bwakila Lukwele IV

WAKATI mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, ukiendelea, Tanzania imeng’ara kimataifa kwa kuwa nchi salama kwa binaadamu kuishi.

Taasisi na mashirika ya habari ya Kimataifa kwenye tafiti za karibuni, imeiweka Tanzania kuwa kinara Afrika mashariki kwa kuwa na Amani na utulivu, kilinganisha na majirani zake.

Bila hiyana hatuna budi kumpongeza Mkuu wa nchi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia misingi iliyoachwa na watangulizi wake ikishadidia upendo baina ya wanajamii, Amani, utulivu, umoja na mshikamano.

Misingi hii iliyokuwepo awamu zote, inaendelea kusimamiwa vizuri na mama yetu (Rais Mheshimiwa Dkt. Samia), na kutupitisha salama kwenye vipindi kadhaa vyenye changamoto nyingi ikiwemo hiki cha uchaguzi.

Uadlifu, haki, upendo, umoja na mshikamano, ndiyo misingi ya uwepo wa Amani na utulivu nchini.

Hivyo ningependa kuwahimiza watanzania wenzangu kulinda na kuienzi misingi hiyo, na kwa dhati kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali anayoiongoza, kwa kusimamia vizuri misingi hiyo.

Binafsi hata hivyo, naona kuna udharula wa kukishajiisha kizazi kichanga, kijue umuhimu wa uwepo wa Amani na utulivu ambavyo ni chachu ya maendeleo.

Wapo Vijana wachache kizazi hiki kipya (‘Generation Z’), ambao hawajui nini maana ya machafuko au vita, tunawasihi ‘wasichukulie poa’ (kirahisi) neno ‘VITA’; wasikubali kushawishiwa na wanasiasa wasiolitakia mema Taifa hili.
Tunawaasa watazame hali ilivyo kwa majirani zetu, sisi pekee tumebaki kuwa KISIWA CHA AMANI na UTULIVU, na kimbilio la hao walioharibikiwa.

Kizazi kichanga, kipo hatarini kuburuzwa kibubusa kwenye giza wasilolijua, kutokana na uzowefu mdogo wa maisha, na upeo finyu wa kuchanganua mambo, na akili nyembamba za kutambua matokeo ya kutenda bila kufikiri kwa kina.

Hivyo, jitihada alizozianza Rais Dkt. Samia hazina budi kuungwa mkono na kila mwananchi, kwa kutoa elimu kubwa zaidi kwa kundi hili muhimu la kijamii kuanzia ngazi ya familia (Mama, Baba, au Mlezi ‘SEMA NA MWANAO’).

Wapo wanaotumia matatizo ya hapa na pale ya vijana, ikiwemo baadhi yao kutokuwa na ajira au mitaji, kuwachochea wavuruge Amani kwa maslahi yao ya kisiasa; lazima tukemee hilo, na kutoa elimu endelevu kwa watoto na vijana wetu.

Kipindi hiki cha Kampeni na hatimae uchaguzi ni wakati wa wanasiasa kunadi sera zao, na kueleza changamoto wanazoziona na namna wanavyoweza kuzitatua; wananchi wakishawishika nao watawapa dhamana ya kuwangoza kwenye nafasi mabimbali (yaani Udiwani, Ubunge au Urais).

Kwa kufanya hivyo, watakuwa wametumia vema majukwaa na pia muda vizuri, pamoja na haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kwa mustakabali mwema wa Jamii yetu; na sio kupanda mbegu mbaya kwa kizazi kichanga hasa cha vijana kwa kuwajaza chuki, na kujenga uhasama, mifarakano, na uwadui, jambo ambalo matunda yake ni vurugu.

Ikumbukwe kuwa, KUNA MAISHA BADAA YA UCHAGUZI ambayo ni marefu zaidi kuliko miezi miwili ya kampeni na siku yenyewe ya kupiga kura.

Ikumbukwe vilevile kuwa, unapopanda mbegu za chuki na uhasama wakati huu kwa kushambuliana binafsi maungoni, badala ya kuvunja na kujenga hoja zenye kuingia akilini mwa wapiga kura; mavuno yake ni hasi na yenye athari mbaya na za muda mrefu baada ya uchaguzi.

Hivi karibuni, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limebainishwa kuwa, Tanzania ndiyo nchi salama zaidi Afrika Mashariki.

Pia, Tanzania imeorodheshwa nafasi ya 73 kwa kuwa nchi salama zaidi kwa kuishi duniani.

Kutokana na tathmini hiyo, Tanzania ina viwango vichache vya uhalifu katika jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ni vema tukaendeleza utamaduni huu unaotufanya kuwa BARUA INAYOSOMEKA kwa wengine.

Mataifa Yasiyo Salama Afrika:-

Wakati Tanzania ikiwa nchi salama zaidi katika jumuiya ya Afrika mashariki, kwa upande wa pili Kenya inaongoza katika taifa lisilo na usalama zaidi, likiorodheshwa nafasi ya 14 barani Afrika.

Uganda nayo ikitajwa nafasi ya 23 kwa nchi isiyo salama, na kuifanya ya pili katika jumuiya ya Afrika mashariki.

“Kusini mwa Jangwa la Sahara imeshuhudia kushuka kwa viwango vya amani katika mwaka uliopita, ambapo wastani wa hali ya amani katika eneo hili umepungua kwa asilimia 0.17” inabainisha taarifa ya BBC.

Ingawa baadhi ya Mataifa yamepiga hatua kuelekea amani, taarifa ya shirika hilo inasema, nusu nyingine ya nchi za eneo hilo zimeendelea kudidimia.

“Kwa sasa, nchi tatu kati ya kumi zenye migogoro mikubwa zaidi duniani zinapatikana Kusini mwa Jangwa la Sahara,” linaeleza rikirejea Ripoti ya Amani ya Dunia ya 2025 (GPI).

Kwa mujibu wa GPI, idadi ya migogoro ya kanda imefikia kiwango chake cha juu zaidi tangu Vita vya Pili vya Dunia, na migogoro mingine mitatu imeibuka mwaka huu pekee.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, JAMUHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO (DRC), inaelezwa kuwa ni moja ya nchi saba hatari zaidi kwa usalama barani Afrika, yenyewe ikiwa kileleni.

“DRC ndiyo nchi inayoongoza kwa ukosefu wa amani katika ukanda huu, na pia imeonesha hali mbaya zaidi kwa mwaka huu.” Imebainishwa na GPI.

Ripoti ya GPI ya 2025 inafichua zaidi kuwa, DRC pia ni miongoni mwa nchi tano zenye hali mbaya kabisa ya amani duniani.

“Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, DRC imeshuhudia kuporomoka kwa viwango vya amani katika nyanja zote kuu za tathmini, na jumla ya upungufu wa asilimia 4.5” ripoti husika inafafanua.

Imeelezwa kuwa, nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa na vita dhidi ya waasi wa M23, kundi ambalo linadaiwa kuungwa mkono na baadhi ya vikosi kutoka Rwanda.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, kuna kati ya wanajeshi 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda wanaoshiriki katika mapigano ndani ya DRC, wakishirikiana na waasi dhidi ya majeshi ya serikali ya Congo.

Kwa upande mwingine, SUDAN KUSINI imeorodheshwa kama nchi isiyo na amani kabisa katika ukanda huu, ikiwa ni ya pili nyuma ya DRC kwa Afrika, na pia ni ya tatu miongoni mwa mataifa yasiyo na amani zaidi duniani.

“Katika mwaka mmoja uliopita, hali ya amani Sudan kusini ilishuka kwa asilimia 0.54, hasa kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya silaha nzito na za nyuklia. Lakini furaha ya kupata uhuru ilitoweka mara baada ya mzozo wa kuwania madaraka kati ya Rais Jenerali Salva Kiir na naibu wake Profesa Riek Machar kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilivyogharimu maisha ya takriban watu 400,000 na kuwalazimu watu milioi 2.5 kukimbia makazi yao” imefafanuliwa.

Hata hivyo, ripoti hsika inasema, mzozo sasa umeanza tena huko pia, huku Umoja wa Mataifa (UN) ukionya kwamba mkataba wa amani wa 2018 kati ya Kiir na Machar unakabiliwa na tishio la kuvunjika.

Imeelezwa zaidi kuwa, Umoja wa Afrika (AU) hadi sasa umeshindwa katika juhudi zake za kurejesha mchakato wa amani, wakati Uganda imetuma wanajeshi wake Sudan Kusini ili kuimarisha nafasi ya Kiir.

Chama cha Bwana Machar kinasema kwamba, hatua hiyo inadhoofisha uhuru wa Sudan Kusini, na makubaliano ya amani ya 2018; ambapo Uganda na serikali ya Kiir zinatetea uamuzi huo wakisema kwamba, inaimarisha makubaliano ya muda mrefu ya usalama kati ya mataifa hayo mawili.

Hata hivyo, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) linawanukuu wadadisi wakisema kuwa, hatua hiyo inaonyesha jinsi nguvu ya Bwana Kiir mamlakani ilivyo dhaifu, huku hofu ikiongezeka kwamba, vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe vinaweza kuanza tena.

Huku hayo yakijiri katika nchi jirani ya SUDAN, vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaendelea kupamba moto, huku Jenerali Hemedt Dagalo akitangaza kuundwa kwa serikali sambamba (Parallel Government).

Hatua yake imekuja licha ya kwamba, vikosi vyake vimepoteza udhibiti wa jiji la Khartoum baada ya mapigano makali, ambapo sasa mji huo umesalia na magofu baada ya majengo yake mengi kulipuliwa kwa mabomu.

Vilevile, ripoti ya Amani ya dunia ya mwaka huu 2025, inaitaja MALI kuwa ni ya Tatu kwa ukosefu Amani Afrika, ambapo hali ya maisha nchini humo imeendelea kuwa ngumu sana, hasa mwezi Julai 2025.

Imebainishwa kuwa, Maeneo kama Timbuktu, Gao, Mopti na Menaka yamekumbwa na ukosefu wa usalama wa muda mrefu.

“Watu wanaishi kwa hofu, huduma muhimu kama afya na usafiri zimevurugika kabisa. Mashambulizi ya silaha, vizuizi vya barabarani, na watu kukimbia makazi yao ni mambo ambayo yamekuwa yakitokea kila siku.” imeelezwa.

Nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika imekumbwa na janga la usalama lililosababishwa na wanamgambo wanaojinasibisha na Uislamu tangu mwaka wa 2012, moja ya sababu zilizotolewa kwa ajili ya kuteka madaraka kijeshi, lakini mashambulizi kutoka kwa vikundi vya wanamgambo wa jihadi yanaendelea na hata kuongezeka.

Hivi karibuni kulikuwa na uvumi kuhusu njama ya mapinduzi ya kijeshi, ambapo mmoja wa Maafisa Jenerali Mohammedine amethibitisha kwamba “wanaoshukiwa kupanga njama ya kutetemesha utawala ndani ya vikosi vya usalama vya Mali” wamewekwa kizuizini kwa kujaribu kuharibu taasisi za jamhuri.”

BURKINA FASO, imetajwa kuwa nchi wa Nne afrika kwa ukosefu wa Amani, ikiwa kwenye mzozo mbaya tangu mwaka 2015, unaochochewa na wanamgambo wa wanaojinasibisha na Uislamu, hasa katika maeneo yake ya kaskazini na mashariki yanayopakana na Mali na Niger.

Uasi huo, ambao awali ulikuwa ni matokeo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Mali mwaka 2012 umezidi, huku vikundi kama Jama’at Nusrat Al-Islam wal Muslimeen (JNIM), Dola la Kiislamu katika Sahara Kuu (ISGS), na Ansaroul Islam wakitumia malalamiko ya ndani, mvutano wa kikabila, na ukosefu wa utawala mzuri kufanya uhalifu.

Kufikia mwaka 2025, takriban asilimia 60 ya eneo la Burkina Faso inaripotiwa kuwa nje ya udhibiti wa serikali, huku vikundi vya wanamgambo vikifanya mashambulizi katika vituo vya jeshi, makazi ya watu, na miundombinu muhimu.

“Kufikia Agosti mwaka huu, zaidi ya watu milioni 2.3 walikuwa tayari wamekimbia makazi yao wengine wakitafuta hifadhi ndani ya nchi, na wengi wakikimbilia mataifa jirani. Familia zimetawanyika, watoto wamekatishwa masomo, na wengi wanaishi kwa hofu ya kesho isiyojulikana” inabainisha Taasisi ya tathmini ya usalama Africa (ASA).

SOMALIA, imetajwa kuwa nchi ya tano barani Afrika ambayo usalama wake ni tete, huku kundi la wanamgambo wa Al-Shabab likitekeleza mashambulizi mabaya kwa kutumia mabomu, kujitoa mhanga, na hata kuwalenga watu maalum kwa mauaji.

Machafuko mengine nchini Somalia yanatokana na migogoro ya kimakabila, hasa katika jimbo la Galmudug, ambako upungufu wa maji, malisho, na ardhi unachochea mapigano.

“Ni hali ya hofu isiyoisha, ambapo hakuna anayehisi yuko salama hata wale wasiokuwa na hatia” imebainishwa.

JAMHURI YA AFRIKA KATI (CAR), ni nchi ya sita kuwa na hai isiyorudhisha ya usalama barani Afrika.

“Raia wa CAR wameendelea kuathirika na mapigano kati ya makundi hasimu, tangu Muungano wa Wazalendo wa Mageuzi (CPC), ushirikiano wa kiholela wa makundi yenye silaha ya uporaji, ulipoanzisha mashambulizi dhidi ya serikali mwishoni mwa mwaka 2020” Ripoti ya BBC imeeleza.

Imefafanua kuwa, mashambulizi hayo yamevuruga makubaliano ya amani ya mwaka 2019, ambayo yalikuwa yamehitimisha rasmi zaidi ya miaka mitano ya vita vya silaha.

NIGERIA, inafunga dimba la nchi saba zisizo na Amani zaidi barani Afrika, ilhali takwimu zilizomo katika ripoti ya Amani duniani 2025 kuhusu “mtazamo wa uhalifu na uzoefu wa ukosefu wa usalama nchini Nigeria” ni za kutisha.

Utafiti huo uliozinduliwa hivi majuzi unaonyesha kuwa, wanamgambo wa Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria, wamerudisha hofu ya enzi ambayo wakazi walidhani imepita.

Hitimisho:-

Taarifa zaidi za utafiti zinaonesha takwimu za kushangaza, ambapo Amani duniani imeendelea kudorora kila mwaka tangu 2014.

Katika kipindi hicho, nchi 100 zimeelezwa kushuhudia kushuka kwa viwango vya amani, huku ni nchi 62 pekee ndizo zilizoboresha hali zao.

Tofauti kati ya mataifa yenye amani kubwa na yale yenye migogoro imezidi kupanuka, ambapo ukosefu wa usawa katika amani umeongezeka kwa asilimia 11.7 katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita.

Nchi 25 zilizo tulivu zaidi zimerekodi kupungua kwa amani kwa wastani wa asilimia 0.5, huku nchi zisizo na utulivu zikiporomoka kwa asilimia 12.2 katika kipindi hicho.

Vifo kutokana na migogoro ya ndani vimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 438 katika miaka 17 iliyopita.

Katika mwaka mmoja uliopita, nchi 75 kati ya zile zilizopimwa na GPI zimeripoti angalau kifo kimoja kutokana na mapigano ya ndani.

GPI inafichua kuwa, hivi sasa, zaidi ya watu milioni 122 wamelazimika kuhama makazi yao kwa nguvu.

Imebainishwa kuwa, kuna nchi 17 ambako zaidi ya asilimia tano ya wakazi wake ni wakimbizi, au watu waliotawanywa ndani ya nchi zao.

Idadi ya waliolazimika kuhama kwa nguvu imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 185, tangu kuanzishwa kwa Kiashiria cha Amani Duniani (GPI).

MAKALA HII IMECHAPISHWA KWENYE VYOMBO KADHAA VYA HABARI HIVI KARIBUNI. MWANDISHI WA MAKALA HII NI CHIFU (PARAMOUNT CHIEF) WA JAMII YA WALUGURU WA HIMAYA YA JADI YA CHOMA, IKIJUMUISHA ENEO KUBWA LA SASA MANISPAA YA MOROGORO, NA MAENEO MACHACHE YA PEMBEZONI MWAKE KIJIOGRAFIA (ZAIDI TEMBELEA WEBSITE: https://lukwelewachoma.or.tz/ au BLOG: http://lukwelewachoma.blogspot.com/); KITAALUMA NI MWANAHABARI NA MCHAMBUZI WA MASUALA YA KIJAMII. KAMA UNA MAONI, MASWALI, AU USHAURI, ANAPATIKANA KWA SIMU NAMBA +255 788 120690, BARUA PEPE: lukwelepace@gmail.com.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here