WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa kiwango cha udumavu miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano nchini kimeshuka kutoka asilimia 48 mwaka 1992 hadi asilimia 30 mwaka 2022.
Ameongeza kuwa, kiwango cha ukondefu miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano kimepungua kutoka asilimia 5 mwaka 1992 hadi asilimia 3.2 mwaka 2022.
Amesema hayo leo Jumanne (Septemba 30, 2025) wakati alipofunga mkutano wa 11 wa wadau wa lishe nchini, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa APC uliopo Bunju Jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua kuwa lishe si suala la kiafya pekee, bali ni nguzo ya maendeleo ya rasilimali watu, uchumi na jamii. “Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na chakula cha kutosha, afya njema na lishe bora”
Kadhalika, Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameendelea kuwa kinara wa mapambano dhidi ya utapiamlo kwa kuhakikisha masuala ya lishe yanapewa kipaumbele kwa kuimarisha bajeti, kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na uhamasishaji wa afua za lishe kuanzia ngazi ya taifa hadi vijijini.